Tariq Ramadhan, mwanafikra wa Kiislamu wa nchini Uswisi amesema kuwa maneno yaliyotolewa hivi karibuni na Papa Benedict XVI kuhusiana na amani ya Mashariki ya Kati hayatoshi na kumtaka achukue hatua za kivitendo kuhusiana na suala hilo.
Kwa muhjibu wa tovuti ya Islamtoday, Ramadhan alizungumzia suala hilo katika mahojiano yake na gazeti la nchini Italia la La Stampa na kusisitiza kwamba, matarajioa au kuomba dua ya amani tu bila kuchukua hatua za kivitendo hakutoshi kuleta amani katika Mashariki ya Kati. Ili kuleta amani ya kudumu katika eneo hili nyeti, Ramadhan amesema kuwa Papa Benedict XVI alipasa kuzungumza na kulaani jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi katika safari yake ya hivi sasa katika ardhi takatifu za Palestina. Amesema kuwa baada ya mauaji ya umati ya siku 22 yaliyotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, Papa huyo anapasa kufahamu kwamba vita hivyo vimevuka mipaka ya kidini na kuingia katika mipaka ya kisiasa. Huku akisisitiza udharura wa kulaaniwa jinai za utawala wa Israel na Papa Benedict, Ramadhan amesema kuwa walimwengu wanamtarajia Papa kuzingatia maadili na kuheshimu makabila tofauti na kuwashinikiza watawala wa Israel ili waheshimu misingi na sheria za kiutu na kimataifa. Amesema kunyamazia kimya jinai za utawala huo kunaweza kuchukuliwa kuwa ni uungaji mkono wa Vatican kwa vitendo vya kinyama vinavyotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia. 404784