Katika maandamano yaliyofanyika huko Ghaza, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesisitiza juu ya kuendelea kutetea na kupigania haki za taifa madhlumu la Palestina.
Wananchi wa Palestina wanaiita tarehe 15 Mei kuwa ni Siku ya Nakba kutokana na kuwa siku hiyo mwaka 1948 ndiyo iliyokuwa siku ya kutangazwa rasmi kubuniwa kwa utawala haramu wa Israel katika ardhi za Wapalestina kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi na hasa Uingereza. Kabla ya kutangazwa rasmi utawala huo, Wazayuni walikuwa wametekeleza njama nyingi za kufukuza mamilioni ya Wapalestina kutoka kwenye ardhi zao za jadi na kuwafanya kuishi kama wakimbizi katika sehemu nyinginezo za dunia na hasa katika nchi jirani. Akizungumzia suala hilo, Fauzi Barhum, Msemaji wa Hamas amesema kuwa, Hamas itaendelea kupigana na Wazayuni hadi pale itakapofikia ushindi wa mwisho kwa kuwafuuza maadui kutoka kwenye ardhi za Wapalestina na kuwarejesha wakimbizi wote wa Kipalestina katika ardhi zao za jadi. Kuhusiana na suala hilo, Baraza Kuu la Palestina siku ya Alkhamisi lilitoa taarifa likisisitiza juu ya ulazima wa kukabiliana na ujenzi wa vitongoji vya Mayahudi katika ardhi za Wapalestina, na hasa katika eneo la Quds Tukufu. Pia limeiomba jamii ya kimataifa kuwasaidia wakimbizi wa Palestina warejee katika ardhi zao za kale. Katika taarifa yake, baraza hilo limesema kuwa Nakba ambayo ilitimia mwaka 1948 kwa Wazayuni kukalia thuluthi tatu ya ardhi ya Wapalestina, kuharibiwa maneo ya makazi 531 na kufukuzwa karibu asilimia 85 ya Wapalestina kutoka kwenye makazi yao, bado inaendelea hadi leo. Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pia siku ya Alkhamisi walifanya maandamano makubwa yaliyowashirikisha shakhsia wengi wa kisiasa, ambao walisisitiza juu ya udharura wa kudumishwa mapambano ya kurudishwa ardhi zote zilizoghusubiwa na Wazayuni wa Israel.
Kuhusiana na suala hilo, viongozi wa Kikristo wapatao 140 wametoa taarifa ambayo ilichapishwa katika gazeti la Independent la nchini Uingereza wakisema kuwa, kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina na utawala haramu wa Israel katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, ndicho chanzo halisi cha matatizo wanayoyapata Wapalestina hao, yakiwemo ya ukimbizi. Mahmoud Abdallah, mmoja wa waandaaji wa kumbukumbu ya 61 ya Nakba pia amesema kuwa, wakolni ndio wahusika halisi wa matatizo yote wanayoyapata Wapalestina na wakati huohuo kukosoa vikali siasa za kuboresha uhusiano na utawala wa Kizayuni zinazotekelezwa na nchi za Kiarabu. Wapalestina wanoishi ndani na nje ya mipaka ya Palestina kila mwaka hukumbuka siku hii ya maangamizi kwa kufanya maandamano na mikusanyiko iliyo dhidi ya Wazayuni na kulaani jinai zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi. 405420