IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu atoa wito wa Umoja na Urafiki katika Umma wa Kiislamu

7:40 - August 10, 2010
Habari ID: 1970258
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amekaribisha suala la kustawishwa uhusiano wa Iran na nchi za Kiislamu na akasema kuwa umma wa Kiislamu ni majmui kubwa yenye vipawa na Waislamu wanapaswa kupeana mkono wa urafiki na umoja popote pale wanapokuwa.
Ayatullah Khamenei ameyasema hayo Jumatatu asubuhi, Agosti 9, 2010, ameonana na Rais Malam Bacai Sanha wa Guinea Bissau, mjini Tehran.
Akieleza jinsi Iran inavyokaribisha ustawishaji wa uhusiano wa Tehran na nchi zote za Kiislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, umma wa Kiislamu ni majimui adhimu yenye vipawa na vipaji vingi na kila alipo Muislamu ana wajibu wa kuwanyooshea Waislamu wenzake mkono wa urafiki na mshikamano.

Ameongeza kuwa, kama ushirikiano kati ya tawala na kati ya mataifa ya Kiislamu utakuwa kwa sura inayotakiwa, bila ya shaka yoyote Waislamu wote duniani watanufaishwa na ushirikiano huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia umuhimu wa bara la Afrika na kuongeza kuwa, mikono ya wakoloni imesababisha matatizo mengi barani Afrika na magharibi mwa bara hilo lakini leo hii mataifa yaliyoamka yameamua kupanua wigo wa ushirikiano baina yao ili kukabiliana na mikono hiyo ya wakoloni.

Ayatullahil Udhma Khamenei vile vile amesema, Iran inakaribisha ushirikiano baina yake na nchi za Afrika na ameongeza kuwa, tofauti na walivyo wakoloni, nchi za bara hilo zinaweza kuihesabu Iran kuwa ni nchi rafiki na ndugu ambayo inaweza kusaidia katika ustawi na maendeleo ya mataifa hayo kwa kuzingatia manufaa ya wananchi wa nchi hizo.

Aidha amezungumzia maendeleo ya kielimu na kiviwanda ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, maendeleo hayo makubwa ya Iran yamepatikana kutokana na moyo na mori wa Kiislamu na kujiamini kitaifa jambo ambalo ni miongoni mwa mafanikio ya Imam Khomeini (Quddisa Sirruh). Amesema, taifa lolote lile linalojijengea sifa ya kujiamini na kuingia vilivyo katika medani ya kazi na juhudi zisizochoka, bila ya shaka yoyote litaweza kupata maendeleo kama hayo.

Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya umuhimu wa kudumishwa amani na utulivu barani Afrika na magharibi mwa bara hilo sambamba na kutiliwa mkazo maendeleo na ustawi wa nchi za bara hilo.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa upande wake Rais Malam Bacai Sanha wa Guinea Bissau amesema kuwa, katika kipindi hiki kifupi cha ziara yake nchini Iran amepata fursa ya kutembelea na kuona kwa karibu baadhi ya maendeleo na uwezo wa kielimu na kiviwanda wa Iran na kwamba amevutiwa na kupigwa na butwaa kutokana na maendeleo hayo makubwa.

Rais Sanha ameongeza kuwa, maendeleo hayo ni ya kustaajabisha na kwamba uwezo na maendeleo ya taifa la Iran ni fakhari kwa mataifa mengine. Amesema nchi yake inaitumia fursa hiyo kustawisha kadiri inavyowezekana uhusiano kati yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
629643
captcha