Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Qatar na kwa ushirikiano wa Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya nchi hiyo. Mkutano huo umefanyika katika fremu ya ratiba maalumu zinazotekelezwa na Qatar katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Mkutano huo pia ni sehemu ya shughuli za mji wa Doha ambao umechaguliwa kuwa mji mkuu wa utamaduni wa nchi za Kiislamu katika mwaka huu wa 2010.
Akizungumza katika mkutano huo, Hassan As-Shafi' mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Yemen amesema kuwa ni wajibu wa kila Muislamu kuitetea Baitul Muqaddas. Ameutaka umma wote wa Kiislamu kufanya juhudi za kukarabati na kuujenga upya mji mtukufu wa Quds pamoja na kuwaunga mkono kwa hali na mali wananchi madhlumu wa Palestina. Akiashiria hali ya kusikitisha ya Baitul Muqaddas kufuatia uharibifu unaofanywa na Wazayuni katika mji huo na hasa dhidi ya Msikiti wa Quds, Muhammad Lutfi as-Swabagh mmoja wa wahadhiri wa masomo ya Kiislamu nchini Saudi Arabia ametahadharisha dhidi ya mipango na njama hatari za utawala haramu wa Israel za kuitokomeza kabisa Baitul Muqaddas na kwamba huo ni mwanzo wa kujengwa hekalu la uongo katika sehemu hiyo takatifu. 633592