Kwa mujibu wa Zinfos 974 hiyo ndiyo tovuti ya kwanza katika bara zima la Ulaya kuwatangazia Waislamu ratiba na amali kama hizo za mwezi wa Ramadhani.
Wakristo wamekuwa wakinufaika na ratiba kama hiyo tokea mwaka 1948 na hadi sasa ni Waislamu tu ndio hawakuwa na mpango kama huo.
Tovuti hiyo huanza kuwatangazia Waislamu ratiba zake tokea saa mbili usiku kwa wakati wa Ufaransa ikiwatangazia shughuli mbalimbali za ibada zinazotekelezwa katika misikiti mbalimbali ya Lyon. Tovuti hiyo imezinduliwa hasa kwa ajili ya kuwanufaisha wagonjwa, walemavu na vijana ambao hawana wakati wa kutosha wa kushiriki katika ibada mbalimbali za mwezi wa Ramadhani misikitini.
Kamil Kabtan, mkuu wa msikiti wa Ijumaa wa Lyon amesema kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa tovuti hiyo ni kueneza mafundisho halisi ya dini ya Kiislamu na kuamiliana na watumiaji wa tovuti hiyo. Kwa maana kwamba watumiaji wa tovuti hiyo wanaweza kuuliza maswali yao kuhusiana na mwezi wa Ramadhani kupitia tuvuti hiyo kabla ya kuwadia wakati wa swala.
Wakuu wa tovuti hiyo wamesema kuwa imefanikiwa kuwavutia watu wengi na kwamba tokea mwanzoni mwa mwezi wa Ramadhani hadi sasa zaidi ya watu 300 wengi wao wakiwa ni Wafaransa, Wamorocco na Wamarekani wameutembelea mtandao huo. Wamesema kuwa tovuti hiyo haitatoa huduma zake katika mwezi huu mtukufu tu bali itaendelea kuwahudumia Waislamu hata baada ya kumalizika mwezi huu kwa kuwaletea ratiba mbalimbali za kiutamaduni kwa lugha za Kifaransa na Kiarabu. 642035