Mashindano ya taifa ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani Tukufu, kuhifadhi hadithi za Mtume Muhammad (saw) na sira ya mtukufu huyo yalianza jana Jumapili tarehe 29 Agosti katika mji mkuu wa Mauritania Nouackchott.
Shirika rasmi la habari la Mauritania limeripoti kuwa mashindano hayo yanawashirikisha washindani 145 na yanasimamiwa na Waziri wa Masuala ya Kiislamu wa nchi hiyo Ahmad Ould al Ladhini.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Miongozo ya Kiislamu cha Wizara ya Masuala ya Kiislamu ya Mauritania Muhammad Old al Shawaf amesema katika hotuba ya ufunguzi wa mashindano hayo kwamba kufanyika mashindano hayo nchini Mauritania ni hatua ya kuwaenzi na kuwahamasisha wasomaji na wahifadhi wa kitabu kitakatifu cha Qur'ani.
Ameongeza kuwa zawadi nono zitatolewa kwa vijana na mabarobaro watakaoshinda nafasi za kwanza hadi tatu kwa lengo la kuwahamasisha kusoma na kutendea kazi mafundisho ya Qur'ani katika nyanja mbalimbali za maisha yao. 644643