Akizungumzia suala hilo hapo siku ya Jumatano katika maonyeso ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu, Hujjatul Islam wal Muslimeen Hamid Muhammadi, Mkuu wa Kituo cha Uratibu na Ustawi wa Shughuli za Qur'ani nchini Iran ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Katika Shughuli za Qur'ani, amesema kuwa bara la Afrika katika miaka ijayo litakuwa katika mstari wa mbele wa kueneza shughuli za Qur'ani duniani. Amesema kutokana na mazingira na nafasi yake nzuri kuhusiana na Qur'ani Tukufu, bara la Afrika katika siku zijazo litakuwa mmbeba bendera halisi wa mapambano dhidi ya dhulma ulimwenguni. Amesema lengo kuu la manabii lilikuwa ni kuwabainishia watu maana halisi ya tauhidi, yaani upweke wa Mwenyezi Mungu na kusimamisha uadilifu miongoni mwao. Amesema kutokana na dhulma liliyofanyiwa bara la Afrika kwa miaka mingi, hivi sasa bara hilo liko mbioni kurejesha haki zake zilizoporwa.
Amesisitiza kwamba kutokana na kuwa Uislamu ambao unapinga dhulma umeenea katika sehemu kubwa ya bara hilo na pia Ushia ambao ni dhihirisho la Uislamu halisi wa kupambana na dhulma duniani umeanza kuenea kwa kasi katika bara hilo, ni wazi kuwa katika miaka ijayo bara hilo litaongoza mabara mengine duniani katika kupigania uadilifu na kupambana na dhulma duniani.
Hujjatul Islam wal Muslimeen Muhammadi ameendelea kusema kuwa kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Waafrika wamekuwa wakizingatia zaidi mafundisho ya Qur'ani Tukufu na kufarijika na kitabu hicho kitakatifu. Amesema kuwa kabla ya ushindi wa Mapinduziya Kiislamu ya Iran Washia wenye asili ya Afrika walikuwa wachache mno lakini hivi sasa idadi yao imeongezeka kwa kasi na kufikia milioni 25 hadi 30. Amesema mustakbali ni wa Waislamu na kwamba idadi kubwa ya watu wasio na dini wamekuwa wakiingia kwa makundi katika dini hii tukufu.
Naibu Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran amesema, hivi sasa kuna madrasa, shule za kawaida, vyuo, vituo vya Kiislamu na vyuo vikuu vya Kiislamu ambavyo vinaendesha shughuli zao za kielimu na Qur'ani katika bara hilo, vituo vya elimu ambavyo katika miaka ijayo vitatoa wanafunzi na wasomi ambao wataongoza harakati kubwa ya kueneza mafundisho ya Qur'ani barani Afrika. 646570