Guido Westerwelle, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema kuwa hatua ya Kasisi Terry Jones wa Florida ya kutaka kuchoma kitabu kitakatifu cha Qur'ani ni ya kiwendawazimu na kwamba ni dharau kubwa dhidi ya jamii ya mwanadamu.
Akizungumza siku ya Jumamosi huko Brussels nchini Ubelgiji, Westerwelle amesema kuwa wito wa kutaka kuchomwa kitabu kitakatifu cha Waislamu ni jambo linalohatarisha usalama wa dunia. Amesema kuwa kitendo hicho alichokitaja kuwa cha kiwendawazimu hakipasi kuruhusiwa kuudhuru Ukristo.
Askofu Terry Jones anayeongoza wafuasi 50 tu wa kanisa lake dogo la Dove World Outreach Center katika jimbo la Florida alikuwa ametoa wito wa kuchomwa Qur'ani siku ya Sptemba 11 ambayo ni siku ya kukumbukwa mashambulio ya kigaidi yaliyotokea mwaka 2001 katika miji ya Washington na New York. Wito huo wa dharau uliamsha hasira kubwa ya Waislamu duniani na hata kuwakera baadhi ya Wakristo walio na misimamo ya wastani. Kasisi huyo hatimaye alilazimika kufutilia mbali mpango huo kutokana na mashinikizo ya Waislamu na fikra za waliowengi duniani. 652560