IQNA

Viongozi wa Kiislamu wa Michigan wataka kufuatiliwa kisheria tukio la kuchomwa Qur'ani

11:25 - September 15, 2010
Habari ID: 1993988
Viongozi wa Baraza la Uhusiano wa Kiislamu na Marekani CAIR tawi la Michigan, wameiomba polisi ya upelelezi ya Marekani FBI kuchunguza na kufuatilia kisheria tukio la kuchomwa Qur'ani katika mji wa Lansing East, lililotekelezwa siku ya Septemba 11.
Kwa mujibu wa tovuti ya Detnews licha ya kasisi Terry Jones kufutilia mbali uamuzi wake wa kuchoma nakala za Qur'ani Tukufu lakini kitabu hicho kilipatikana kimechanwa na kuchomwa moto karibu na Kituo cha Kiislamu cha mji wa Lansing.
Dawoud Walid, mkurugenzi mkuu wa tawi la Michigan la baraza la CAIR amesema jambo hilo linakinzana na misingi ya uhuru wa kuabudu na ni ishara ya wazi ya taasubi za kidini. Wasimamizi wa baraza hilo katika mji wa Lansing wamesema kuwa waliifahamisha polisi ya eneo hilo uwezekano wa kutokea matukio kama hayo ya dharau dhidi ya Qur'ani lakini haikuchukua hatua yoyote ya kukabiliana na wahalifu wanaokosea heshima kitabu hicho. Amesema dharau hiyo imewaathiri sana wakazi wa mji huo na hata wasiokuwa Waislamu, kwa kadiri kwamba wakazi hao wakiwemo Wahindu, Wayahudi na Wakristo wamejitolea kuokota na kukusanya kurasa zilizochanwa na kupeperushwa na upepo katika sehemu mbalimbali za mji huo na kuzirejesha katika chuo hicho cha Kiislamu. 653614
captcha