IQNA

Mawakili wa Misri wafanya mgomo wa kukaa chini kulalamikia kuchomwa Qur'ani

17:19 - September 21, 2010
Habari ID: 1998858
Mawakili kadhaa wa Misri jana Jumatatu tarehe 20 Septemba walifanya mgomo wa kukaa chini kwa lengo la kulalamikia kitendo cha dharau cha baadhi ya watu nchini Marekani cha kuchoma moto Qur'ani Tukufu.
Kwa mujibu wa gazeti la Misri la al-Yaum as-Sabe', mawakili hao walilalamikia vikali kitendo hicho na kusema kuwa hatua ya Terry Jones ya kutoa wito wa kuchomwa Qur'ani Tukufu ni ya kitaasubi na inayovuka mipaka ya mantiki na akili. Wamesema mafundisho ya Kiislamu yanashajiisha ushirikiano, urafiki na kuishi pamoja kwa amani jamii na mataifa mbalimbali licha ya itikadi na mitazamo yao tofauti, na kwamba kamwe Uislamu hauruhusu taasubi na fikra za kupindukia mipaka.
Katika mgomo huo, Hamdi Khalifa, Katibu wa Jumuiya ya Mawakili wa Misri, amesema kuwa lengo la dharau na uadui huo dhidi ya Uislamu ambao umekuwepo katika kipindi chote cha historia, ni kufuta utambulisho halisi wa Waislamu. Amesema, kuuawa shahidi nchini Ujerumani Marwa al-Sherbini, mwanamke wa Kimisri kutokana na hijabu na Uislamu wake ni moja ya athari mbaya za misimamo hiyo ya kupindukia mipaka ya Wamagharibi dhidi ya Uislamu.
Mwishoni Hamdi Khalifa amewataka viongozi na watawala wa nchi za Kiislamu kufanya juhudi za kuzuia kukaririwa kwa vitendo kama hivyo vya dharau dhidi ya Qur'ani na Uislamu katika nchi za Magharibi. Pia amewataka walimwengu kukabiliana na watu wanaotumia mabavu dhidi ya wenzao walio na mitazamo na imani tofauti. 660055
captcha