IQNA

Kikao cha kimataifa cha kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu kufanyika mjini London

12:21 - September 22, 2010
Habari ID: 1999273
Kikao cha nne cha kimataifa cha kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu kimepangwa kufanyika tarehe 3 Oktoba mjini London Uingereza. Kikao hicho kimeandaliwa na Kituo cha Kiislamu cha Uingereza.
Kituo hicho ambacho tayari kimeandaa vikao vingine vitatu kama hicho kimepanga kuandaa kikao cha nne chini ya anwani ya 'nafasi ya ukuribishaji madhehebu ya Kiislamu katika harakati ya umma wa Kiislamu na ujenzi wa mustakbali.'
Wasimamizi wa kikao hicho wamesema kuwa vikao kama hivyo vina umuhimu mkubwa kwa kuzingatia udharura wa kuimarisha na kueneza utamaduni wa kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu miongoni mwa Waislamu.
Kikao cha maswali na majibu cha waandishi habari na wasomi pamoja na wanafikra watakaoshiriki katika kikao hicho kitafanyika pambizoni mwa kikao hicho cha London.
Huku wakitoa wito kwa wanazuoni na wasomi wa Kiislamu kushiriki kwa wingi katika kikao hicho, wasimamizi wa kikao hicho wamesema kuwa kikao cha mara hii kina umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani hali tata inayotawala hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Wamesema washiriki wa kikao hicho watatakiwa kuchukua misimamo madhubuti ya kuboresha umma wa Kiislamu na kukabiliana na changamoto muhimu zinazowakabiliwa Waislamu. 660149
captcha