Fatuwa ya Ayatullahil Udhma Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya kuharamisha kumkosea heshima Bibi Aisha, mke wa Mtume Mtukufu (saw) na shakhsia wengine wa Kiislamu wanaoheshimiwa na Masuni, imepokelewa vizuri na maulama pamoja na wanazuoni wa ulimwengu wa Kiislamu, kikiwemo chuo kikuu cha kidini cha al-Azhar cha mjini Cairo.
Fatuwa hiyo imejadiliwa na kuchambuliwa na vyombo vingi vya habari vya nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Ahmad at-Tayyib, Sheikh wa al-Azhar ametoa taarifa akimshukuru Ayatullah Ali Khamenei kwa kuharamisha kukosewa heshima masahaba na wake wa Mtume (saw). Ameongeza kuwa fatuwa hiyo inaonyesha wazi kudiriki vyema Kiongozi Muadhamu hatari inayoenezwa na wafitini dhidi ya Uislamu na kwamba inathibitisha pia kwamba Kiongozi Muadhamu anafuatilia kwa karibu juhudi za kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.
Huku akisisitiza kwamba Chuo cha al-Azhar kinawataka Waislamu wote, bila kujali tofauti ya rangi na madhehebu zao, kuzingatia umoja na mshikamano, Sheikhul al-Azhar amesisitiza kuwa kila mtu anayewasha moto wa fitina miongoni mwa Waislamu huwa amefanya dhambi na kwa hivyo anastahiki kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu na kufukuzwa miongoni mwa Waislamu.
Sheikh Ahmad At-Tayyib amesema kuwa jambo muhimu ni kwa Waislamu wote duniani kuzingatia umoja na mshikamano na kupunguza mivutano na hitilafu zinazoweza kugawa na kuudhuru umma wa Kiislamu.
Fatuwa hiyo ya Kiongozi Muadhamu pia imejadiliwa na kuchambuliwa kwa kina na televisheni muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu ya al-Jazeera ambayo imezingatia zaidi athari za umoja za fatuwa hiyo miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya Waislamu. Tunakumbusha hapa kuwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamanei ametoa fatuwa hiyo kufuatia swali lililotolewa na kundi moja la wanazuoni wa eneo la Ihsaa la nchini Saudi Arabia, kufuatia matamshi ya dharau yaliyotolewa hivi karibuni na Yassir al-Habi wa Kuwait dhidi ya Bibi Aisha, mke wa Mtume (saw).
Maulama na wanazuoni wa Kishia katika nchi za Saudi Arabia, Iran na nchi nyinginezo za Ghuba ya Uajemi wamelaani matamshi hayo ya al-Habib dhidi ya Aisha. 668172