Abdul Aziz al-Tuweijri, Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Nchi za Kiislamu ISESCO amesisitiza huko Tunis Tunisia udharura wa kuanzishwa kituo madhubuti cha upashaji habari kwa Waislamu kuhusiana na umuhimu wa kulindwa mazingira duniani.
Akizungumza katika kikao cha nne cha Mawaziri wa Mazingira wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ambacho kimekuwa kikiendelea huko mjini Tunis Tunisia tokea siku ya Jumanne, al-Tuweijri amesema kuwa kikao hicho kimefanyika katika mazingira ambayo ulimwengu mzima unazingatia zaidi suala la kulindwa mazingira na manufaa yake kwa jamii ya mwanadamu.
Amesema kulindwa mazingira kwa kutegemea miongozo ya kielimu na katika fremu ya ushirikiano wa kimataifa ni hatua muhimu katika kulinda jamii ya mwanadamu dhidi ya matukio na mabalaa ya kimaumbile, kimazingira, kiuchumi na kijamii.
Rais Zeinul Abideen bin Ali wa Tunisia na Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ni miongoni mwa watu waliozungumza katika kikao hicho.
Mawaziri wa mazingira wa nchi 57 wanachama wa OIC na vilevile wawakilishi wa jumuiya 30 za Kiislamu za Kimataifa zinazojishughulisha na masuala ya mazingira wameshiriki katika kikao hicho cha siku mbili ambacho kimechunguza njia na mbinu za Kiislamu za kukabiliana na athari mbaya za ongezeko la joto na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. 669660