'Sote tunyanyue haki', ni nara itakayoongoza kikao cha mwaka huu cha Umoja wa Idhaa na Televisheni za Nchi za Kiislamu, kikao ambacho kimepangwa kuanza rasmi hapa mjini Tehran siku ya Jumamosi ijayo.
Kujadiliwa masuala ya ndani ya umoja huo, kuwasilishwa ripoti kuhusiana na shughuli zilizofanyika katika kipindi cha mwaka mzima na kupasishwa mipango ya shughuli zijazo ni miongoni mwa mambo yatakayochunguzwa na Baraza Kuu la umoja huo katika siku chache zijazo.
Akizungumzia suala hilo katika mkutano wa waandishi habari jana Jumatano, Hujjatul Islam Walmuslimeen, Ali Karimiyan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Idhaa na Televisheni za Kiislamu amesema kuwa umoja huo ulioanzishwa rasmi mwaka uliopita umepata mafanikio makubwa ya kuimarisha ushirikiano kati ya wanachama wake ambao wanaendesha shughuli zao za upashaji habari kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu na suna za Mtume Mtukufu (saw). Amesema malengo muhimu ya umoja huo ni 1- kuimarisha shughuli za uandishi na upashaji habari kwa msingi wa kielimu, udugu na utu. 2- Kuimarisha ushirikiano katika nyanja za utamaduni, dini na siasa kwa madhumuni ya kuunufaisha umma wa Kiislamu na kukabiliana na kila aina ya ubaguzi, ukafiri, ukoloni na hujuma ya kiutamaduni. 3- Kutumia vyombo vya habari katika kutetea matukufu ya kidini na kuufahamisha ulimwengu mafundisho halisi ya Uislamu na suna za Mtume (saw). 4- Kutetea haki za mataifa na jamii za Kiislamu na kuziunga mkono mbele ya unyanyasaji wa mabeberu na Wazayuni pamoja na kufanya juhudi za kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu na kuimarisha utambulisho wa Kiislamu miongoni mwao. 5- Kuunga mkoni na kusisitiza uchapishaji wa vitabu na majarida yanayohimiza utambulisho wa Kiislamu, kufanya juhudi za kuleta mfumo wa kiuadilifu ulimwenguni, mfumo ambao utalinda haki na maendeleo ya tamaduni zote.
Hujjatul Islam Walmuslimeen Karimiyan amesema, kwa kuwa na mashirika ya idhaa na televisheni zaidi ya 200 kutoka nchi 30 za dunia umoja huo ndio pekee ulio na wanachama katika mabara yote ya dunia. 669988