IQNA

Safari ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Qum ni ya Kihistoria

13:46 - October 23, 2010
Habari ID: 2017360
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema safari ya kihistoria ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Qum ni ishara ya umuhimu wa mji huo kama kituo na sehemu yalipozaliwa Mapinduzi ya Kiislamu.
Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Seddiqi akihutubu katika sala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran ameashiria safari ya Ayatullahil Udhma Khamenei katika mji mtakatifu wa Qum na kusema, 'safari hii imepelekea ulimwengu kuelekeza macho katika kituo cha Mapinduzi ya Kiislamu na makao ya kueneza dini na elimu ya Kiislamu'.
Akihutubia waumini katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran, Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Seddiqi amesema nasaha za Kiongozi Muadhamu alipowahutubia wanachuo wa vyuo vya kidini na wanazuoni ni hati ya kiakhlaqi, kisiasa, kijamii, kielimu na ya vyuo vya kidini. Amesisitiza umuhimu wa kuchambua kwa kina hati hiyo.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema kujitokeza kwa wingi wananchi wa matabaka mbalimbali mjini Qum katika kumkaribisha Kiongozi Muadhamu kunakumbusha mapokezi ya kihistoria ya Imam Khomeini MA aliporejea Iran kutoka Paris mwaka 1979. Amesema mapokezi makubwa ya Kiongozi Muadhamu huko Qum yanaashiria kuwa kiongozi wa Kiislamu na wilaya ya kidini ni kivuli kilichojaa baraka na watu wote wanahisi haja yake.
Kwingineko katika hotuba yake, Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Seddiqi ameashiria safari ya Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran nchini Lebanon na kuitaja kuwa moja ya karama za Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesema pamoja na kuwepo njama za maadui za kuitenga Iran safari hiyo inaonyesha kuwa nuru ya mfumo wa Kiislamu wa Iran iko katika nyoyo za umma na inazidi kuenea kote duniani.
captcha