IQNA

Viongozi wa Kiislamu na Kikristo kuchunguza wasiwasi wa pamoja wa kidini

12:09 - October 28, 2010
Habari ID: 2021223
Viongozi na wanazuoni wa Kiislamu na Kikristo wanatazamiwa kukutana katika Kituo cha Baraza la Kimataifa la Makanisa huko Geneva Uswisi tokea tarehe Mosi hadi Nne Novemba kwa ajili ya kuchunguza wasiwasi wao wa pamoja kuhusiana na masuala ya kidini.
Kikao hicho kitakachofanyika chini ya anwani ya 'Ubadilishwaji wa Jamii, Ujenzi wa Mustakbali wa Pamoja wa Waislamu na Wakristo', kitajadili wasiwasi huo na kuutafutia ufumbuzi wa pamoja ili kuimarisha shughuli za Kiislamu na Kikristo katika pembe mbalimbali za dunia.
Watakaohutubia kikao hicho ni pamoja na Qadhi bin Muhammad bin Talal, mwakilishi maalumu wa Mfalme Abdallah II wa Jordan, Kasisi Andres Wajrid kutoka Kanisa la Sweden na Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimtaifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu kutoka Iran.
Washiriki wa kikao hicho watatembelea misikiti na makanisa mashuhuri ya Geneva na pia kukutana na viongozi wa jumuiya za kidini katika mji huo. Kwa Ujumla wazungumzaji 60 wamepangiwa kuhutubia kikao hicho. 683918
captcha