Hammarberg amesema kwamba ni wazi kuwa iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kwa wakati, suala hilo huenda likazusha mivutano ya kikabila na kijamii na kuchochea matatizo mengi katika uwanja huo.
Akitoa ripoti kuhusiana na muamala mbaya wa kisiasa unaofanywa dhidi ya Waislamu wa Ulaya, Hammarberg ameashiria kupigwa marufuku ujenzi wa minara ya misiki nchini Uswisi na nchi nyingine za Ulaya na kusema kuwa vitendo vya aina hiyo vinathibitisha wazi kuwepo chuki, hofu bandia, dhana mbaya na taasubi hasi dhidi ya Waislamu na utamaduni wao barani humo. Ameendelea kusema kuwa, Waislamu wa Ulaya wanakabiliwa na aina mbalimbali za ubaguzi wanapokuwa masokoni, makazini na mashuleni katika nchi za Ulaya na kusisitiza kwamba hilo ni tatizo kubwa la ukiukaji wa haki za binadamu linalopaswa kushughulikiwa haraka iwezekanavyo katika nchi hizo.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanyika hivi karibuni nchini Ujerumani yanaonyesha kuwa asilimia 58 ya wananchi wa nchi hiyo wanaamini kwamba shughuli za kidini za Waislamu zinapaswa kubanwa zaidi nchini. Hammarberg amesema jambo hilo linatokana na chuki, ujinga, propaganda hasi dhidi ya Waislamu na kuenezwa hofu dhidi ya utamaduni wa Kiislamu, jambo ambalo amesema, viongozi wa kisiasa wa Ulaya hadi sasa wamezembea katika kukabiliana nalo.
Kati hali ya hivi sasa, karibu Waislamu milioni 1.6 wanaishi Uingereza, milioni 3.8 nchini Ujerumani, milioni 5 Ufaransa na kati ya milioni 15 hadi 20 nchini Russia. Wengi wa Waislamu hao walizaliwa na kukulia katika nchi hizohizo.
Licha ya ukweli huo lakini bado Waislamu hao wanabaguliwa kwa njia mbalimbali katika nchi hizo na hivyo kuhisi kuwa raia wa daraja la pili.
Baraza la Ulaya lililo na nchi wanachama 47 ni taasisi kubwa zaidi ya haki za binadamu na demokrasia barani Ulaya na ina makao makuu yake katika mji wa Strasbourg nchini Ufaransa. Hiyo ni taasisi huru isiyotegemea Umoja wa Ulaya. 685773