Wanafikra na wasomi 66 wa Kiislamu kutoka nchi za Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain wametoa taarifa ya pamoja wakitaka mbinu za pamoja zichukuliwe kwa lengo la kupambana na fitina za kimadhehebu na kusimama imara dhidi ya siasa za kibaguzi.
Taarifa hiyo imezitaka baadhi ya serikali za Mashariki ya Kati kukomesha mara moja siasa zao za ukiukaji wa haki za binadamu, uvunjaji wa heshima za watu, uhuru wa kusema na kuondoa marufuku ya safari za baadhi ya shakhsia.
Taarifa hiyo imesisitiza juu ya umuhimu wa kufanyika mazungumzo muhimu na chanya kati ya taasisi mbalimbali za kiraia, kidini na kiutamaduni za nchi za eneo hilo kwa ajili ya kutafuta njia za kutatua matatizo ya hivi sasa na yajayo ya umma wa Kiislamu.
Wanafikra na wasomi hao wa Kiislamu wamebainisha wazi wasiwasi wao kuhusiana na kuongezeka wimbi la fitina na machafuko ya kimadhehebu na kikabila katika jamii za Kiislamu na kuongeza kuwa, jambo hilo limeimarisha harakati za kupindukia mipaka na za kuwakufurisha Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu.
Watu waliotia saini taarifa hiyo wamesisitiza kwamba kutolewa kwa maoni yasiyo ya kimantiki na ya dharau dhidi ya matukufu ya kidini na madhehebu ya Kiislamu kumechangia pakubwa katika kueneza chuki na kutoaminiana miongoni mwa Waislamu. 686482