IQNA

5:59 - November 04, 2010
Habari ID: 2025318

Tuzo ya kimataifa ya 'Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu' yaanzishwa Sweden

Jumuiya ya Kimataifa ya Sayansi na Utamaduni ya Sweden imechukua hatua muhimu ya kuanzisha tuzo ya kwanza ya kimataifa ya utamaduni iliyopewa jina tukufu la 'Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu'.

Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa ya Sayansi na Utamaduni ya Sweden imesema kuwa taasisi hiyo imeanzisha tuzo mbili zilizopewa jina la "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Tuzo ya Uhuru". Imesema kuwa tuzo ya Muhammad (saw) ni ya kwanza kuanzishwa katika uga wa kimataifa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Taasisi ya Kimataifa ya Saansi na Utamaduni ya Sweden imeainisha vigezo na malengo kwa ajili ya tuzo hizo ambazo zitakuwa zikitolewa kila mwaka kwa watu wanaofanya harakati za kubainisha mafundisho aali na halisi ya ujumbe wa Uislamu na wito wa Nabii Muhammad (saw) na kuchukua hatua za kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa mbalimbali, kupambana na dhulma, umaskini na ujinga na kuzuia dharau dhidi ya matukufu.
Taasisi ya Sayansi na Utamaduni ya Sweden imesema kuwa tuzo ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu ya mwaka huu wa 2010 itatolewa kwa Emil Sarsour ambaye ni Mwenyekiti wa Muungano wa Jumuiya za Wahajiri katika mji wa Upssala nchini Sweden kutokana na jitihada zake kubwa za kudhihirisha taswira nzuri ya Waislamu.
Imesema kuwa tuzo ya Uhuru ya mwaka huu ya jumuiya hiyo itatolewa kwa mwanahistoria wa Sweden Matias Gardil kutokana na mapambano yake kwa njia za amani dhidi ya watu wanaopuuza dini na kuwatishia wenzao kuhusu dini ya Kiislamu na Waislamu.
Sherehe za kutolewa tuzo hizo itafanyika tarehe 19 Novemba katika mji wa Upssala ikihudhuriwa na shakhsia wa kisiasa na wanahabari.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi na Utamaduni ya Sweden iliasisiwa mwaka 2009 katika mji wa Upssala nchini Sweden na kazi yake ya kwanza na muhimu zaidi ni kuanzisha tuzo ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu inayokusudia kumuarifisha mtukufu huyo kwa alimwengu. 687907

captcha