Sayyid Swadru Deen al-Qubanchi, Imam wa Swala ya Ijumaa ya mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq amesisitiza juu ya umuhimu wa siku ya Arafa na pia umuhimu wa Waislamu kuzuru haram ya Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) katika siku hiyo.
Akizungumza katika swala ya Ijumaa ya mji huo Sayyid Qubanchi amesema kuwa kwa mujibu wa hadithi za Ahlul Beit (as) Mwenyezi Mungu katika siku hii tukufu kabla ya kuwatazama watu waliokusanyika katika uwanja wa Arafa huwatazama watu wanaozuru kaburi na haram ya Imam Hussein (as). Sayyid Qbanchi pia amezungumzia makumbusho ya tukio la kuuawa shahidi Imam Muhammad Baqir (as) na kusema kuwa Mtume Mtukufu ndiye aliyempa lakabu ya Baqir yaani mchanua elimu.
Pia amezungumzia tukio la Taf na kuongeza kuwa Muslim bin Aqil ndiye aliyekuwa shahidi wa kwanza wa vita hivyo vya Karbala.
Imam wa Swala ya Ijumaa ya mji mtakatifu wa Najaf amezungumzia pia matukio ya kigaidi yaliyotekelezwa hivi karibuni dhidi ya Mashia katika miji ya Najaf, Karbalaa na Basra na kusisitiza kwamba matukio hayo kamwe hayatadhoofisha moyo na irada ya Wairaki ya kutaka kufikia maendeleo na ustawi katika nchi yao. 694288