IQNA

Ushirikiano wa serikali ya Ugiriki kwa ajili ya kujengwa msikiti wa kwanza mjini Athens

11:21 - December 06, 2010
Habari ID: 2043063
Ujenzi wa msikiti wa kwanza mjini Athens kwa lengo la kukidhi mahitaji ya ibada ya wakazi Waislamu wa mji huo utapata kasi kubwa hivi karibuni baada ya serikali ya Ugiriki kukubali kushirikiana na Waislamu ili kufikia lengo hilo.
Kwa mujibu wa gazeti la Ta Nea linalochapishwa mjini Athens, serikali ya Ugiriki imekubali kutenga bajeti ya kujengwa msikiti wa muda katika eneo lililokuwa likimilikiwa na kikosi cha wanamaji wa nchi hiyo katika mji wa Athens kabla ya kushughulikia ujenzi wa msikiti mkubwa wa kwanza na wa kudumu ambao utakuwa na uwezo wa kubeba watu 500 katika eneo hilohilo kufikia mwaka 2012.
Maelfu ya wahajiri Waislamu kutoka nchi za Kiarabu, Kiafrika na India wamekuwa wakiishi nchini humo kwa miaka mingi bila ya kuwa na sehemu maalumu ya kutekelezea ibada zao wala hata makaburi maalumu ya kuzika maiti zao. Hii ni katika hali ambayo serikali tofauti za nchi hiyo zimekuwa zikitoa ahadi nyingi zisizotekelezwa kwa Waislamu kuhusu jambo hilo.
Hadi sasa Waislamu wa Ugiriki wamekuwa wakikodi sehemu au kutekelezea ibada zao katika sehemu zilizoachwa wazi jambo ambalo limekuwa likihatarisha usalama wao kutokana na vitendo vya wabaguzi wa nchi hiyo.
Katika siku ya Idul Adh'ha ya mwaka huu, Waislamu waliosimamisha swala ya idi katika mji wa Athens walifanyiwa vitendo vya kejeli na dharau na baadhi ya wakazi wa mji huo na hata kutishiwa usalama wao na baadhi ya mirengo ya kibaguzi na yenye misimamo ya kupindukia mipaka. 707001
captcha