IQNA

Rais Ahmadinejad: Njia ya mwanadamu kuelekea kwenye uhuru inapitia Palestina

15:58 - December 14, 2010
Habari ID: 2047604
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameshiriki katika hafla ya ya kuupokea msafara wa Asia unaopeleka misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wa Ghaza wanaozingirwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa 'njia ya mwanaadamu kuelekea kwenye uhuru inapitia Palestina'.
Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa Palestina ni kioo kinachoakisi sura halisi ya hali ya mwanadamu wa dunia ya sasa na historia ya miaka iliyopita ya kiumbe huyo.
Ameongeza kuwa hii leo imeeleweka wazi kwamba utawala mtendajinai wa Israel ulianzishwa kwa mujibu wa ratiba maalumu ya kudhibiti dunia likiwemo eneo la Mashariki ya Kati.
Amesema kuwa utawala wa Kizayuni uliasisiwa kwa shabaha ya kulidhibiti eneo la Mashariki ya Kati na dunia nzima na kudumisha mipango ya ukoloni na wakoloni. Amesema kuwa jinai zote za madola ya kibeberu zinafanyika hii leo huko Palestina. Amesisitiza kuwa utatuzi wa kadhia ya Palestina na kung'oa mizizi ya Uzayuni ni wajibu wa wanadamu wote na watu wa rangi, kaumu, makabila, mirengo mbalimbali na dini zote za Mwenyezi Mungu na wote wanawajibika kushikana mkono na kukomesha tatizo hilo kubwa zaidi la mwanadamu wa leo.
Rais Ahmadinejad ameuambia msafara wa Asia unaoelekea Ghaza kwamba harakati yao ni sawa na mche mchanga wa mti ulioota katika kiwiliwili cha ubinadamu na utachanua na kustawi zaidi kwa kukombolewa Palestina. Rais Ahmadinejad amesisitiza kuwa, 'taifa la Iran liko pamoja na wote wanaotetea uhuru na uadilifu duniani'.
Msafara wa Asia unaobeba misaada ya kibinadamu kwa ajili ya raia wa Ghaza umelakiwa na maelfu ya wananchi wa jiji la Tehran baada ya kupita katika miji kadhaa ya Iran ukitokea Pakistan. Msafara huo ulianzia India na unatazamiwa kupitia Uturuki na Misri na kisha kuwasili Ghaza mwishoni mwa mwezi huu wa Desemba.
712287
captcha