IQNA

Kikao cha pamoja cha shakhsia wa Kishia na Kisuni chafanyika Madina

12:52 - December 25, 2010
Habari ID: 2052655
Kikao cha kuimarisha umoja na mshikamano kati ya shakhsia wa Kishia na Kisuni kimefanyika mjini Madina kwa uungaji mkono wa Amir wa mji huo Abdul Aziz bin Majid.
Kikao hicho kilifanyika siku ya Jumatano kufuatia matukio ya kusikitisha yaliyotokea mjini Madina siku ya Ashura ambapo kundi moja la Mawahabi wenye misimamo ya chuki dhidi ya Ushia lilishambulia makundi kadhaa ya waombolezaji wa mauaji ya Imam Hussein (as).
Akizungumza katika kikao hicho, Abdul Aziz bin Majid ameelezea masikitiko yake kutokana na mashambulio hayo katika siku ya Ashura ya mwaka huu na kuongeza kuwa Uislamu ni dini inayopinga kila aina ya chuki na mifarakano ya kimadhehebu. Amewaonya watu wanaojaribu kuvuruga amani mjini humo na kuwaomba wanafikra wa Kishia na Kisuni waandae kikao cha kitaifa ili wawasihi wafuasi wao wajaribu kuondoa mivutano inayoshuhudiwa kati ya pande mbili hizo.
Tunakumbusha hapa kuwa katika siku ya Ashura ya mwaka huu mjini Madina kundi moja la Mwahabi wenye misimamo ya kupindukia mipaka na chuki dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia lilivamia na kushambulia kundi moja la Washia waliokuwa wakiomboleza mauaji ya Imam Hussein (as) katika mji huo ambapo watu kadhaa walijeruhiwa na mali ya umma kuharibiwa. Hatimaye ghasia hizo zilizimwa na askari usalama baada ya kutiwa nguvuni watu 50. 717426
captcha