Naibu Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislami siku ya Alkhamisi alimtumia barua Yusuf Qardhawi mkuu wa muungano huo akibainisha malalamiko yake makubwa kuhusu kuchapishwa kitabu kilicho dhidi ya Ushia kwa jina la 'at-Tashayu fi Afriqiya' ambacho kina mambo mengi yaliyo dhidi ya Ushia.
Katika barua hiyo, Ayatullah Waidhzadeh Khorasani, Naibu Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu, amesema kuwa kitabu hicho kilipaswa kuchunguzwa kwa makini na bodi ya wadhamini wa muungano huo kabla ya kuchapishwa. Amesema watu walioandika kitabu hicho hawakuwa na habari sahihi wala za kutosha kuhusiana na walichokuwa wakikiandika na hivyo kuamua kutumia mbinu za chuki na kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Waislamu wa Kishia.
Ayatullah Khorasani amelalamikia vikali mbinu ya kishetani iliyotumika katika uandishi wa kitabu hicho ambayo amesema ndicho chanzo cha kutokea matukio ya kusikitisha na machungu katika ulimwengu wa Kiislamu na hasa barani Afrika dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema baadhi ya vituo vya Kishia vilivyotajwa kwenye kitabu hicho havina uhusiano wowote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wala haviafikiani nayo kifikra kwa kiwango kikubwa. Amesema hii ni katika hali ambayo Mashia pia wana haki ya kujishughulisha kwa uhuru kamili na shughuli zao mbalimbali za kiutamaduni na kimadhehebu na kujenga misikiti na vituo vyao vya utamaduni katika sehemu tofauti duniani.
Ayatullah Waidhzadeh Khorasani amesisitiza kwamba majukumu ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Iran yanatekelezwa ndani ya nchi kwa ajili ya kuoanisha utamaduni wa Kiirani na mafundisho ya Kiislamu na wala sio nje ya nchi. 730142