Katika kikao kilichofanyika hapo siku ya Jumatatu, bunge la Iraq likiongozwa na Spika Usama an-Nujaifi limetaka taasisi zote muhimu za kimataifa ikiwemo Vatican, Marekani na Umoja wa Mataifa kulaani vikali kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu huko Marekani na Kasisi Terry Jones.
Wabunge hao wapatao 164 wa Iraq wametaka pia mwaka huu uitwe kuwa mwaka wa kutetea Qur'ani. Wametaka kufuatiliwa na kuhukumiwa kisheria kwa wale wote wanaothubutu kukosea heshima kitabu hicho kitakatifu. Wamesema kuwa kitendo hicho ni dharau ya wazi dhidi ya matukufu ya Mwenyezi Mungu na kukitaja kuwa aina ya ugaidi wa kifikra. Wamekemea vikali kitendo cha nchi nyingi za Kiislamu cha kunyamazia kimya kitendo hicho cha aibu na dharau dhidi ya matukufu ya Kiislamu kilichofanywa na watu wasofahamu vyema mafundisho ya kidini huko Marekani. Marekani pia imetakiwa imtie mbaroni na kumpa adhabu kali kasisi huyo mwovu aliyehusika na kitendo hicho cha kuchoma moto Qur'ani Tukufu. Katika upande wa pili, Umoja wa Mataifa umetakiwa kubuni sheria itakayoharamisha dharau kama hiyo dhidi ya vitabu vya mbinguni na kulinda utukufu wavyo. Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC imetakiwa kuandaa kikao cha dharura kwa lengo la kuchunguza njia za kufuatiliwa kisheria wahalifu wa kitendo hicho. Baadhi ya wabunge pia wametaka balozi wa Marekani nchini humo afukweze hadi serikali ya Washington itakapowaomba radhi rasmi Waislamu kuhusiana na kitendo hicho cha chuki za Wamarekani dhidi ya Uislamu. 769063