IQNA

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu yafanyika Ufaransa

12:06 - April 07, 2011
Habari ID: 2101963
Waislamu wa Ufaransa wamefanya maandamano makubwa mbele ya makao makuu ya chama cha UMP kwa ajili ya kulalamikia kuongezeka vitendo vya chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Saphirnews maandamano hayo yameitishwa na jumuiya ya wananchi wanaopinga chuki dhidi ya Uislamu CECI. Jumuiya hiyo inasema kuwa vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vimeongezeka sana katika miji mingi ya Ufaransa na hasa Lyon na vilevile katika nchi nyingine za Ulaya. Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo imesema kuwa Uislamu umekuwa ukilengwa katika nchi za Ulaya na hasa Ufaransa kwa njia mbalimbali yakiwemo masuala ya hijabu, vyakula halali vya Kiislamu, utambulisho wa Waislamu, swala katika maeneo ya wazi, vitabu vya waandishi, bunge, idara za serikali na pia kupitia vyombo vya habari vya nchi hizo. Waislamu wanasema hujuma kubwa ya ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu imekuwa ikendeshwa ili kuonyesha kuwa Uislamu ndio unaovuruga usalama na kueneza ugaidi nchini Ufaransa katika hali ambayo ukosefu wa ajira, uonevu katika idara za serikali dhidi ya Waislamu na ufisadi ndiyo matatizo makuu ya nchi hiyo. Maandamano kama hayo yalifanyika siku ya Jumamosi mjini Paris kulaani chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo. 768640
captcha