IQNA

Kiongozi Muadhamu: Mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa utakuwa na mafanikio

16:02 - April 24, 2011
Habari ID: 2111140
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa hivi sasa Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika utapata ushindi na kuwa na natija nzuri.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumamosi asubuhi, Aprili 23, 2011, aliponana na maelfu ya wananchi wa mkoa wa Fars wa kusini mwa Iran na kutoa hotuba muhimu sana mbele yao.
Huku akibainisha hali nyeti inayoikabili dunia na eneo hivi sasa kutokana na kuongezeka mwamko wa Kiislamu, amewataka wananchi na viongozi wote wa Iran kulinda umoja na mshikamano baina yao na kufanya kazi kwa idili na bidii isiyosita ili wasitoe mwanya wowote kwa maadui wa utawala wa Kiislamu.
Aidha amesisitiza kwa kusema: Leo hii mihimili mitatu mikuu nchini na hasa Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhudumia taifa kwa dhati kabisa na kwamba wananchi na Kiongozi Muadhamu nchini siku zote wanaunga mkono uchapaji kazi na kuitumikia nchi lakini kila mahala ambapo Kiongozi Muadhamu atahisi kumesahauliwa maslahi makubwa zaidi lazima ataingilia kati na madhali yuko hai kamwe hataruhusu harakati adhimu ya taifa la Iran ya kuelekea kwenye malengo yake makuu matukufu yaende kombo hata kwa chembe moja.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kusimama kidete taifa la Iran juu ya misimamo yake ya haki na kuwa kwake kigezo cha mataifa mengine ya eneo ndiyo sababu kuu ya kushuhudiwa mashinikizo na propaganda za chuki dhidi ya utawala wa Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa: Licha ya kuweko mashinikizo yote hayo lakini utawala wa Jamhuri ya Kiislamu umeendelea kusimama imara bila ya kulegalega na kwamba uimara huu wa utawala wa Kiislamu ndio uliopelekea kushindwa kikamilifu uadui wao.
Amesisitiza kwamba taifa na serikali ya Iran inabidi iulinde umadhubuti huu wa utawala wa Kiislamu unaofanana na umadhubuti wa jabali na kuongeza kuwa: Msiruhusu kutokea mifarakano na hitilafu kwani kwa njia hiyo litakuja kufanikiwa lile ambalo adui analipigia chapuo katika propaganda na ukhabithi wake wa kisiasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria juu ya matukio ya siku za hivi karibuni nchini Iran na kuhusu Wizara ya Usalama wa Taifa nchini na kuongeza kuwa: Oneni propaganda za vyombo vya maadui kuhusiana na suala hili ambalo hata halina umuhimu wa hivyo, lakini angalieni jinsi vyombo hivyo vilivyopiga propaganda kubwa na kulitolea uchambuzi wa kila namna jambo hilo dogo, wanasema katika Jamhuri ya Kiislamu kumetokezea mfarakano na utawala wa aina mbili unaokinzana na Rais wa nchi hiyo sasa hata hasikilizi tena maneno ya Kiongozi Muadhamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Propaganda za maadui katika siku za hivi karibuni kwa mara nyingine zimeonyesha ni kitu gani hasa kinasubiriwa na maadui hao na jinsi walivyokaa na kuvizia mithili ya mbwa mwitu wakisubiri kupata upenyo mdogo tu washambulie.
Aidha amesisitiza kuwa, kwa haki na kwa insafu inabidi tuseme kwamba serikali na Rais mwenyewe wanahudumia taifa kwa udhati wa moyo wao na kuongeza kuwa: Taifa na Kiongozi Muadhamu siku zote wanaunga mkono uchapaji kazi na kulitumikia taifa na wala kigezo wanachotumia si sura za watu bali kigezo kikuu ni kazi na huduma kwa taifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa kazi na majukumu yote yamebainishwa vizuri katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kwa kusema: Kiongozi Muadhamu kamwe hakujipangia kuingilia maamuzi na kazi za serikali ila pale atakapohisi kuna maslahi ya taifa yamefumbiwa macho.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Katika kadhia ya hivi karibuni ambayo nayo hata si muhimu kiasi hicho, ilionekana kwamba kuna maslahi makubwa yamefumbiwa macho (na ndio maana ilibidi Kiongozi Muadhamu aingilie kati).
Vile vile amewausia wahusika wakuu na watu wenye uchungu na nchi wajiepushe na maneno-maneno ya pembeni na uchambuzi chapwa unaotolewa dhidi ya kila mmoja wao na wala wasitoe mwanya wa kuathiriwa na propaganda za maadui na kusisitiza kwamba: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni chombo chenye nguvu kubwa na Kiongozi Muadhamu naye amesimama imara juu ya misimamo sahihi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Hadi ambapo nitakuwa hai na nitakuwa na cheo basi kamwe sitaruhusu harakati adhimu ya taifa la Iran ya kuelekea kwenye matukufu yake ipotoshwe na kupelekwa kombo hata kwa sekunde moja. Mwenyezi Mungu ataendelea kulisaidia taifa la Iran madhali wananchi wataendelea kuweko kwenye medani wakiwa na hamasa, hisia za kupenda nchi yao, tabasuri na muono wa mbali pamoja na azma na nia ya kweli isiyotetereka.
Ameongeza kuwa: Kama viongozi nchini watajipeleka kwenye masuala yao binafsi na kusahau majukumu yao, basi msaada wa Mwenyezi Mungu nao utapungua.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Leo hii mbali na wananchi, viongozi katika mihimili mitatu ya dola (yaani Serikali, Mahakama na Bunge) nao wanaendelea kutekeleza majukumu yao mazito kwa juhudi, bidii na uchapaji kazi mkubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia suala la kutangazwa mwaka huu wa Kiirani wa 1390 Hijria Shamsia kuwa mwaka wa "Jihadi ya Kiuchuni" na kusisitiza kwamba: Wananchi na viongozi wote nchini wanapaswa kushirikiana ili kuhakikisha kuwa harakati hii inaanza kwani lengo la kupewa jina kila mwaka ni kuandaa mazingira ya kuanza harakati kuelekea kwenye ufanikishaji wa kaulimbiu na lengo lililokusudiwa.
Amesisitiza kuwa, wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola si kwamba hawana dosari katika kazi zao lakini amekumbusha kuwa: Inabidi kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu wakati wote na sambamba na kujiidilisha kugundua nuksani zao, wafanye juhudi za kuzipunguza ili wasije wakaleta vizuizi katika harakati ya taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matukio yanayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kuongeza kuwa: Leo hii kwa baraka za Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu kumetokezea mwamko mkubwa wa Kiislamu katika eneo ambapo bila ya shaka yoyote harakati hizo zitafanikiwa tu kama ambavyo tayari zimeshafanikiwa katika baadhi ya nchi za eneo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kadiri watu wanavyozidi kuwa na azma ya kweli, imani na kuwa tayari kujitoa muhanga katika njia yao ndivyo uwezekano wa kupata ushindi unavyozidi kuongezeka.
Vile vile ameashiria kuemewa Marekani, Ulaya na Wazayuni mbele ya mabadiliko ya eneo na kuongeza kuwa: Madola ya kibeberu yanafanya juhudi zao zote kuhakikisha kuwa yanadhibiti mabadiliko ya eneo lakini mwamko huu wa Kiislamu si kitu cha kuweza kumalizika bali harakati hii inazidi kusonga mbele na kamwe haitarudi nyuma.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hatima na mustakbali wa harakati hii utakuwa ni kwa manufaa ya wananchi wa eneo hili lakini wakati huo huo wanananchi hao wanapaswa kuwa macho na makini sana kwani adui anavizia hivi sasa ili akipata fursa ndogo tu aitumie kupotosha harakati hii.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia juu ya dhulma wanayofanyiwa wananchi wa Bahrain, Yemen na Libya na kusisitiza kuwa: Tathimini ya kiinsafu kuhusiana na matukio ya hivi sasa ya eneo na hasa katika nchi hizi tatu inaonyesha kuwa, madola ya Magharibi yamewadhulumu wananchi wa nchi hizo na madola hayo ya Magharibi ni wakosa na watenda jinai ambao hawapasi kufumbiwa macho.
Amesema, sababu kuu inayoifanya Marekani na nchi za Magharibi ziwadhulumu wananchi wa eneo hili ni utawala pandikizi wa Israel na kukumbusha kuwa: Watu waliofanyiwa dhulma kubwa zaidi katika matukio ya hivi sasa ya eneo ni wananchi wa Bahrain.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia juu ya propaganda kubwa zinazofanywa na nchi za Magharibi dhidi ya Iran na kuongeza kuwa: Madola ya Magharibi yameelekeza zaidi mashambulizi yao ya kipropaganda dhidi ya Iran kutokana na kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeamua kuwa na misimamo ya haki na kuitangaza hadharani misimamo yake hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tofauti na yanavyotaka madola ya kiistikbari, haiangalii kwa macho tu mabadiliko ya eneo hili na kwamba wananchi, serikali na shakhsia muhimu wa kisiasa nchini Iran kamwe hawatakaa kuangalia kwa macho tu vitendo vya dhulma vya mabeberu.
Aidha ameashiria juu ya madai kwamba eti Iran inaingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo na kusema kuwa madai hayo hayana msingi wowote. Ameongeza kuwa, ilichofanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kutangaza wazi tu msimamo wake na haiingilii kivyovyote vile masuala ya ndani ya Bahrain, Yemen na wala Libya.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Hakuna wakati hata mmoja ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewahi kushughulishwa na kufutuka madola yenye nguvu bandia na kwamba katika siku za usoni pia haitatishwa na madola hayo na wala haitashughulishwa nayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbusha kuwa: Ni haki na ni mahala pake wananchi wa Bahrain kuonyesha upinzani wao na kama kila mtu mwenye muono mpana atabainishiwa hali ya wananchi wa Bahrain na jinsi serikali yao ilivyo na namna watawala wanavyotumia vibaya utawala wao, basi bila ya shaka yoyote atalaani vitendo vya utawala wa nchi hiyo.
Ameongeza kuwa: Hatua zinazochukuliwa na serikali ya Bahrain kukabiliana na wananchi ni makosa kwani hatua kama hizo hazina faida yoyote ghairi ya kuongeza chuki na hasira za wananchi na kuna uwezekano hasira za wananchi zikazuka tena kwa nguvu kubwa zaidi kiasi kwamba serikali isiweze kufanya kitu chochote kingine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa: Mbali na serikali ya Bahrain, watu ambao wametoka nje ya nchi hiyo na kupeleka vikosi vyao huko Bahrain nao wamefanya kosa kubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, matukio ya Libya nayo ni mfano mwingine wa dhulma ya madola ya kiistikbari dhidi ya wananchi wa eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kuongeza kuwa: Wamagharibi hawataki kuona serikali ya wananchi na ya Waislamu inaingia madarakani katika nchi ya Libya ambayo iko karibu na Ulaya na ina utajiri mkubwa wa mafuta, hivyo wameamua kuwachezea tamthilia na mchezo wa kisiasa wananchi wa Libya lakini wananchi hao wameshazigundua siasa hizo za Wamagharibi.
Amesema wakosa wakuu katika matukio ya hivi sasa ya eneo ni mabeberu wa dunia na kanali ya Uzayuni wa kimataifa na kuongeza kuwa: Maadui hao wanatumia hali iliyojitokeza hivi sasa kuzidi kuwashinikiza wananchi wa Ghaza na kuwaua shahidi raia kila leo, hivyo inabidi mataifa ya eneo na tawala za nchi za eneo zisifumbie macho vitendo vya utawala wa Kizayuni.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria historia kongwe na nzuri sana ya maulamaa na wananchi wa mkoa wa Fars nchini Iran hususan mji wa Shiraz katika nyuga mbali mbali za mapambano, jihadi, kushikamana na dini, isimu na fasihi na masuala mengine ya kisiasa na kijamii na kuongeza kuwa: Siku zote wananchi wa Fars wako mstari wa mbele katika mambo yote na kwamba mkoa wa Fars kwa haki na insafu ni jabali hasa.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia heshima kubwa inayoongezeka kila leo ambayo wananchi wa Fars wanaipa Haram ya Ahmad bin Musa na ndugu wa mtukufu huyo na hatua ya wananchi wa mkoa huo ya kutoa mashahidi kumi na nne elfu na mia sita katika kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran) na kuutaja kuwa huo ni mfano wa wazi wa kushikamana na dini na kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu wananchi wa mkoa huo na kusisitiza kuwa: Siri kuu ya mafanikio ya mataifa mbali mbali ni kusimama kidete kwenye neno lao la haki na kutokana na kuwa taifa la Iran limesimama imara kwenye njia yake liliyojichagulia, mbali na kujipatia maendeleo ya kila leo katika nyuga tofauti limeweza pia kuwa kigezo kizuri kwa mataifa mengine.
Katika mkutano huo Hujjatul Islam Walmuslimin Imani, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala na Imam wa Ijumaa wa mji wa Shiraz amesema katika hotuba yake kwamba kuweko Haram ya Tatu ya Ahlul Bayt mjini Shiraz, maulamaa wakubwa wa mkoa wa Fars, nafasi ya wananchi katika kipindi cha mwamko wa Kiislamu na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuweko mashahidi 14,600 wa mkoa wa Fars waliomwaga damu zao katika kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu ni miongoni mwa sifa maalumu na kubwa za wananchi wapenda dini na fasihi wa mkoa wa Fars.
Aidha katika mkutano huo kamanda wa jeshi la Sepah mkoani Fars ametoa ripoti juu ya kufanyika kongamano kubwa la mashahidi 14,600 wa mkoa wa Fars.
779661
captcha