IQNA

Baraza la Maaskofu wa Ufaransa lakosoa siasa za serikali ya Paris dhidi ya Waislamu

17:10 - April 27, 2011
Habari ID: 2113325
Askofu Mgr Podvin, Msemaji wa Baraza la Maaskofu wa Ufaransa CEF amekosoa siasa za serikali ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu.
Akizungumza na televisheni ya Europe 1, msemaji wa baraza hilo la maaskofu wa Kanisa Katoliki ameashiria kutoandaliwa maeneo yanayofaa kwa ajili ya Waislamu kutekelezea ibada zao na kusema kuwa Waislamu wanalazimika kuswali katika maeneo ya wazi na mabarabara ya miji ya nchi hiyo kutokana na kutoandaliwa nafasi za kutosha za kutekelezea ibada zao. Amesema kutokana na ukweli huo watu wasiokuwa Waislamu nchini humo hawapasi kuwatuhumu Waislamu na kuwahusisha na mambo yasiyofaa.
Ameashiria matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Claude Gueant, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa aliyedai kuwa Waislamu wanahatarisha usalama wa nchi hiyo kutokana na kuongezeka kwa idadi yao nchini, na kusema kuwa kama kweli Wafansa wanataka kuwa na nchi huru na ya kidemokrasia wanapasa kuwasilisha misimamo yao kwa njia tofauti na kujiepusha kuwatuhumu wenzao na masuala yasiyo na ukweli wowote.
Askofu Podvin amesema mwishoni kwamba mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo yamekuwa yakiendelea nchini humo kwa muda wa miaka 30 sasa bila ya kuathiriwa na masuala ya kisiasa na kuongeza kuwa maisha ya amani kati ya pande mbili hizo yanawalazimu wafauasi wao kuvumiliana na kudumisha udugu na urafiki miongoni mwao. 782265
captcha