IQNA

Utawala wa Israel na Marekani; tishio kubwa zaidi kwa jamii ya Kiislamu

13:48 - May 03, 2011
Habari ID: 2116467
Sayyid Hassan an-Nimr, mwanafikra na msomi mashuhuri wa Kiislamu anayeishi katika mji wa Saihaat nchini Saudi Arabia amesema kuwa utawala haramu wa Israel na Marekani ndio hatari kubwa zaidi inayoikabili jamii ya Kiislamu.
Amewaambia watawala wa Saudia kuwa iwapo wanatambua wakati huu kuwa wakati mgumu zaidi kwao katika mtazamo wa masuala ya kiusalama, wanapasa kushughulia kwa karibu mahitaji na matakwa ya wananchi wao.
Akiashiria kuongezeka kwa maandamano na malalamiko ya wananchi katika nchi hiyo na nchi nyingine za Kiarabu, imam huyo wa Swala ya Ijumaa ya mjini Saihaat amesema kuwa wananchi wa nchi hizo watavuka kipindi hiki kigumu cha machungu na mateso wanayotwishwa na watawala waovu wa nchi hizo na kwamba wanazuoni watakuwa katika mstari wa mbele wa kuzima fitina na migogoro inayozikumba nchi hizo. Ameashiria matamshi yanayotolewa na baadhi ya wanazuoni wasioelewa ukweli wa mambo na kuyataja kuwa ni ya kusikitisha. Amesema wanazuoni hao waovu hutamka mambo kama kwamba hawana elimu yoyote ya kimsingi kuhusiana na mafundisho ya Kiislamu. Amesikitishwa na hali ya kuwa baadhi ya watu hao wanaotajwa kuwa ni wanazuoni na wajuzi wa masuala ya Kiislamu wanatoa matamshi ya kibaguzi, kikabila na kimadhehebu ambayo yanakwenda kinyume moja kwa moja na misingi ya mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Amesema matamshi na mielekeo hiyo inayobainisha ufinyu wa fikra zao imewafanya wasiweze kutambua wala kutofautisha kati ya dhalimu na mdhulumiwa.
Hata hivyo ameongeza kuwa kuna baadhi ya watu wanaojiweka kwenye hali hiyo ya kusikitisha kwa makusudi na kutambua vyema mambo wanayofanya kwa maslahi ya maadui wa Uislamu. 784905
captcha