Nadhir al-Mu'mani, daktari wa meno raia wa Jordan ameshinda zawadi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya muujiza wa kielimu wa Qur'ani Tukufu na suna za Mtume yaliyofanyika hivi karibuni huko katika Chuo Kikuu cha al-Azhar nchini Misri, kwa kuwasilisha utafiti juu ya muujiza wa kielimu wa takbiratul ihram.
Kwa mujibu wa gazeti la ad-Dastur linalochapishwa nchini Jordan, daktari huyo pia amefanikiwa kupata zawadi ya nne ya mashindano hayo kwa kuwasilisha makala kuhusu elimu ya anga za mbali.
Kuhusiana na suala la takbiratul ihram, Dokta al-Mu'mani anabainisha faida za kitendo hicho cha kiibada kwa kusema kuwa Muislamu anapofanya takbiratul ihram, kwa muda wa sekunda chache tu, damu iliyobeba hewa ya oksijeni na chakula huweza kufika kwenye ubongo wake na kwamba jambo hilo lina umuhimu mkubwa katika kudhibiti mapigo ya moyo, kuratibu mfumo wa kupumua, kuimarisha mzunguko wa damu mwilini na kutuliza magonjwa kama vile ya shinikizo la damu.
Katika utafiti huo, Dokta al-Mu'mani anasema kuwa mja anapoinua juu mikono yake wakati anapofanya takbiratul ihram, zaidi ya mililita 83.3 za damu husukumwa na moyo hadi kwenye viungo vya juu ya mwili ukiwemo ubongo, katika kipindi cha sekunde moja tu, na kuongeza kuwa hiyo ni rekodi ya kushangaza ya ufikishaji damu kwa kasi ya juu, rekodi ambayo amesema haijawahi kuonekana sehemu yoyote katika taaluma ya tiba. Amesisitiza kwamba hadi sasa hakuna dawa yoyote ambayo imeweza kugunduliwa duniani ambayo ina uwezo kama huo wa kudhibiti mapigo ya moyo na kuufanya ufikishe damu kwa kasi kama hiyo ya juu kwenye viongo mbalimbali vya mwili.
Daktari huyo wa Jordan pia anasema katika utafiti wake kwamba hadi sasa hakuna dawa ambayo imegunduliwa duniani iliyo na uwezo wa kuathiri ubongo kwa kiwango kikubwa kama hicho kinachotokana na takbiratul ihram wakati wa ibada ya swala. 786423