Akizungumzia suala hilo hapo jana Jumatano, Ayatullah Abdul Amir Qabalan, amesema mapatano hayo ni hatua muhimu sana katika kufikiwa malengo ya Wapalestina, malengo ambayo amesema yanahitajia juhudi maradufu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba stratejia ya Palestina moja yenye nguvu inapatikana katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na walowezi wa Kizayuni.
Ayatullah Qabalan ametaka kuimarishwa ushirikiano kati ya makundi yote ya Palestina ili kuilinda Palestina kutokana na vitisho vya utawala haramu wa Israel.
Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Mashia wa Lebanon amesisitiza pia juu ya udharura wa makundi hayo kufanya juhudi za kuondoa kabisa mambo yanayozusha tofauti baina yao na kuongeza kuwa Wapalestina wote wanakabiliwa na hatima moja kutoka kwa adui wao mmoja ambaye wanawajibika kushirikiana kwa lengo la kupambana na njama zake. Amesema utawala ghasibu wa Israel daima unafanya juhudi za kuyahudisha ardhi za Wapalestina na kuharibu Msikiti wa al-Aqswa na kwamba kwa msingi huo Wapalestina wote wanapasa kuishi kwa umoja chini ya bendera ya mapambano ili kukabiliana na malengo ya adui Mzayuni.
Ameelezea matumaini yake kwamba amani na umoja utadumu katika ulimwengu na kuwataka wanafikra na wasomi wa Kiislamu kueneza utamaduni wa ushirikiano kati ya Waislamu ili udugu na ushirikiano uchukue nafasi ya chuki na fitina miongoni mwao kwa madhumuni ya kuulinda umma wa Kiislamu kutokana na shari pamoja na vitisho vya maadui wake. 786879