IQNA

Waandishi 250 wa Saudia wataka wafungwa wa kisiasa waachiwe huru

16:58 - May 11, 2011
Habari ID: 2120425
Waandishi na wasomi 250 wa Saudi Arabia wameitaka serikali ya nchi hiyo kuwaachilia huru mara moja wafungwa 180 waliotiwa nguvuni katika maandamano ya hivi karibuni nchini humo.
Wakitoa taarifa kuhusu suala hilo wasomi hao wameutaka ufalme wa nchi hiyo kutafuta njia bora za kutatua mara moja tatizo la wafungwa hao waliotiwa nguvuni kutokana na kubainisha mtazamo wao wa kisiasa na kiitikadi.
Wafungwa hao wa kisiasa walitiwa mbaroni hivi karibuni katika eneo lenye Washia wengi la Qatif. Wasomi hao wamesema kuwa siasa zinazotekelezwa na utawala wa Saudia za kuwatia nguvuni wasomi ni aina moja ya fitina na wameutaka utawala huo kusimamisha siasa hizo za ukandamizaji mara moja.
Waliotia saini taarifa hiyo wamebainisha wazi wasiwasi wao kuhusiana na hatua ya askari wa nchi hiyo ya kutumia nguvu za ziada dhidi ya wasomi na wanafikra wa wanaolalamikia kwa njia ya amani hali mbaya ya kisiasa ya nchi hiyo.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita maeneo ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ya mashariki mwa Saudia yamekuwa yakishuhudia maandamano makubwa ya amani yanayoandaliwa kwa ajili ya kulalamikia ubaguzi wa kimadhehebu na ukandamizaji wa kisiasa unaofanywa na watawala wa Riyadh dhidi ya Mashia na kutaka wafungwa wao wa kisiasa waachiliwe huru mara moja. 789336
captcha