Zaghlul Najjar, Mkuu wa Kamati ya Muujiza wa Kielimu wa Qur'ani ya Misri amesema kuwa kuanguka kwa utawala wa kidikteta na kitaghuti wa Hosni Mubarak nchini Misri ni moja kati ya alama za nguvu na kudra ya Mwenyezi Mungu duniani.
Akizungumza hivi karibuni katika kikao cha kuchunguza mapinduzi ya Januari 25 nchini Misri, Zaghlul ameashiria kuenea kwa dhulma na ufisadi nchini Misri katika kipindi cha uongozi wa Mubarak na kusema kuwa utawala wa dikteta huyo ulikuwa wa kishetani. Aongeza kuwa katika kipindi cha utawala huo wanafiki mafisadi walinufaika sana na utawala huo huku wananchi wa Misri wakiteseka chini ya sheria ya hali ya hatari nchini.
Huku akisema kuwa katika utawala huo wananchi daima walikuwa wakipata machungu ya matatizo ya kiuchumi na umasikini, Zaghlul amesisitiza kwamba Wamisri wamekuwa wakipata maudhi makubwa kutokana na kutokuwepo uadilifu wa kijamii nchini. Amesema dikteta Mubarak alifanikiwa kuwakandamiza wananchi wa Misri kwa miaka mingi kutokana na siasa zake za kueneza ufisadi, kupotosha fikra za watu, kuwafuta kazi viongozi wa kidini wasioafikiana naye na kuwatumia vibaya wale waliokubali kunufaika na siasa zake hizo mbovu. 801492