IQNA

Imam Jawad AS alihimiza juu ya udharura wa kupata radhi ya Mwenyezi Mungu

16:50 - June 13, 2011
Habari ID: 2137415
Mmoja kati ya nyota za Ahlul Bayt wa Mtume SAW, Imam Jawad AS alizaliwa siku kama ya leo mwaka 195 Hijria Qamariya katika mji wa Madina. Mtukufu huyo alisifika kwa kuwa na elimu kubwa, fasaha na balagha yake.
Tokea utotoni alikuwa na uwezo usio na kifani katika elimu, hekima na fasihi. Kila mmoja katika Ahlul Bayt wa Mtume SAW alijitahidi katika zama zake kutumia mbinu inayokubalika zaidi ili aweze kufikisha ujumbe wake kwa njia bora.
Ucha Mungu ndio uliokuwa msingi wa maisha ya watukufu hawa. Kwa hivyo walizingatia sana masuala kama vile kutekeleza uadilifu na usawa, kumuokoa mwanadamu kutoka kwenye utumwa wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kurekebisha uhusiano wa mtu na jamii.
Japokuwa watukufu hawa hawakufanikiwa kuanzisha serikali katika aghalabu ya wakati, lakini kwa mtazamo wao madaraka na vyeo vilipaswa kuwa chombo cha kuleta uadilifu, haki , kuvunja batili na kueneza dini ya Mwenyezi Mungu. Watukufu hawa waliweza kutawala nyoyo za watu kwa vitendo na amali zao kutokana na kuwa walikuwa kielelezo cha thamani za mwanadamu na maadili bora. Tunatoa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa nyota hii katika anga ya Ahlul Bayt wa Mtume SAW.
Imam Jawad AS alizaliwa siku kama ya leo tarehe 10 Rajab mwaka 195 Hijria Qamariya katika mji wa Madina. Mtukufu huyo alisifika kwa kuwa na elimu kubwa, fasaha na balagha. Tokea utotoni alikuwa na uwezo usio na kifani katika elimu, hekima na fasihi. Maisha na Uimamu wake ulienda sambamba na utawala wa khalifa wa kiimla wa silisila ya Bani Abbas yaani Maamun na Muutasim. Kutokana na kuwa makhalifa wa Kiabbasi hawakuheshimu wala kuekeleza mafundisho ya Kiislamu na walizingatia tu masuala ya kidhahiri, walilenga kubadilisha hukumu za kidini na kuzusha bidaa katika mafundisho ya kidini.
Majibu na upinzani wa Imam Jawad AS kwa sera hizi potofu uliakisiwa kwa kiwango kikubwa na hivyo kupelekea Imam na wafuasi wake kusumbuliwa na kubughudhiwa na watawala wa Kiabbasi.
Imam Jawad AS, kama walivyokuwa Ahlul Bayt wengine wa Mtume SAW, hakunyamaza kimya mbele ya dhulma, ukatili na hadaa ya watawala wa Bani Abbas kwa umma. Mtukufu huyo alibainisha ukweli kwa umma katika mazingira magumu zaidi.
Imam Jawad AS alisimama kidete kwa ushujaa na bila kutetereka katika kukabiliana na dhulma na ukandamizaji wa watawala wa Bani Abbas. Misimamo ya Imam huyu mtukufu ilikuwa imara kiasi kwamba watawala wa Bani Abbas hawangeweza kumvumilia na hivyo wakaamua kumuua shahidi mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka 25.
Miongoni mwa juhudi kubwa za kiutamaduni za Imam Jawad AS ilikuwa ni kunukulu hadithi sahihi za Mtume SAW pamoja na kubainisha njia nyoofu ya Ahlul Bayt wake.
Imam Jawad AS, kupitia njia ya kunukulu hadithi za Mtume SAW aliweza kueneza utamaduni na mafundisho yenye uhai ya kidini katika jamii. Vilevile kwa kuzingatia zama na kwa mujibu wa mahitajio ya kifikra na kiutamaduni ya umma, alitoa hotuba kuhusu maudhui mbalimbali.
Moja ya suluhisho lililotolewa na Imam Jawad AS la kutekeleza mafundisho ya Mwenyezi Mungu, ni kuanzisha uhusiano mkubwa baina ya umma na Qur’ani Tukufu.
Imam aliamini kuwa aya za Qur’ani zinapaswa kuenezwa kwa kiasi kikubwa katika jamii ili Waislamu waweze kunufaika na mafundisho yake.
Imam Jawad AS aliamini kuwa kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu ndio ufunguo wa saada ya mwanadamu katika dunia na akhera. Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’ani aliamini kuwa kumridhisha na kumfurahisha Mwenyezi Mungu ni muhimu zaidi ya kila kitu. Katika Suratu Tauba aya ya 72 tunasoma kuwa: ‘Mwenyezi Mungu amewaahidi waumini wanaume na waumini wanawake bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na makaazi mema katika bustani za kudumu, na radhi za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa’
Ni kwa msingi huo ndio maana Imam Jawad AS aliwataka watu wafikirie tu suala la kumridhisha Mwenyezi Mungu.
Katika moja ya semi zake zenye thamani, Imam Jawad AS anasema:
‘Vitu vitatu vinamfurahisha Mwenyezi Mungu: Kwanza ni kufanya istighfari na kuomba msamaha wa Mwenyezi Mungu. Pili ni kuwa mkarimu na tatu ni kutoa sadaka kwa wingi. (Musnad Al Imam Jawad Uk 742)
Moja ya neema za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu ni istighfari na tauba. Kwa kweli tauba na istighfari ni moja kati ya milango ya rehma za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Kwa tauba na kurejea kwa Mola Muumba, madhambi yaliyotangulia hufutwa na mwanadamu hupata fursa nyingine ya kuziba pengo la mabaya yaliyotangulia. Fursa mpya baada ya mwanadamu kutubu hupatikana kupitia kufanya amali njema na hivyo kuusafisha na kuutakasa moyo wake.
Ni kwa sababu hii ndio maana haipaswi kuchelewesha tauba kwani kinyume na hili ni majuto.
Tauba ni kuomba kusamehewa. Hii inamaanisha kuwa mwanadamu anamtaka Mwenyezi Mungu amsamehe na amjaalie kuwa kati ya wanaopata rehma zake. Kuhusu hili Imam Ali AS anasema: ‘Katika ardhi kuna njia na nyenzo mbili za kupata salama kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Moja yazo ni kuwepo Mtume SAW ambayo iliondoka kwa kuaga dunia mtukufu huyo, na ya pili ni istighfari. Njia hii ipo kwa ajili ya watu wote hadi Siku ya Kiyama. Kwa hivyo itafuteni na shikamaneni nayo.
(Nahjul Balagha, Hekima No 88)
Istighfari inaweza kumuondolea mwanadamu adhabu za dunia na akhera, ili kama alivyosema Imam Jawad AS, mwanadamu aweze kupata radhi ya Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa aya za Qur’ani Tukufu, kati ya athari muhimu zaidi za istighfari ni kuzuia adhabu za Mwenyezi Mungu, kusamehewa dhambi na kuongeza rizki na umri.
Ukarimu ni moja ya njia ambazo Imam Jawad AS alisema zinaleta radhi ya Mwenyezi Mungu. Imam Jawad AS alisema, njia ya kwanza ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu ni istighfari yaani kurekebisha uhusiano wa mwanadamu na Mwenyezi Mungu. Kisha katika sehemu ya pili na ya tatu ni kuhusu uhusiano wa mwanadamu na wanadamu wenzake. Yaani njia ya kumfurahisha Mwenyezi Mungu inapatikana kwa kuwahudumia viumbe wa Mwenyezi. Uhusiano huu unapaswa kuandamana na ukarimu. Bila shaka ukarimu hupelekea kuwepo unyenyekevu na kumuweka mbali mwanadamu na kiburi. Hii ni kwa sababu kiburi ndio chanzo cha dhulma na na tabia ya kuwakandamiza watu wengine.
Imam Jawad AS amesema njia ya tatu ya kumridhisha Mwenyezi Mungu ni kutoa sadaka yaani kuwafanyia hisani wanadamu. Mtukufu huyo binafsi alikuwa katika mstari wa mbele katika jambo hilo na ndio sababu akapewa lakabu ya Jawad, yaani mtu karimu mno. Kwa hivyo Imam Jawad AS aliwataka wanadamu kufuata njia ambayo yeye mwenyewe alikuwa amepata uzoefu wa kuipitia na kuona athari zake nzuri. Kutoa na kuwapa sadaka wengine ni jambo ambalo limehimizwa sana katika Qur’ani Tukufu.
Wapenzi wasikilizaji tunachukua fursa hii kutoa tena salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Jawad AS na tunakamilisha makala hii kwa kunufaika na miongozo yake. Kama unavyojua baadhi ya watu hutafuta fakhari na heshima kupitia utajiri, madaraka, kaumu na rangi zao na kwa kuwadharau wasio na sifa hizo. Lakini Imam Jawad AS anasema, heshima na hadhi halisi ni elimu ambayo ni mapambo ya mwanadamu na kwamba ukubwa na adhama hutokana na fadhila za kimaanawi na kiroho. Katika moja ya hotuba zake alisema: ‘Sharifu wa kweli ni mtu ambaye amejipamba kwa elimu, na mtu mwenye adhama na saada halisi ni yule anachukua mkondo wa taqwa na kumjua Mwenyezi Mungu’.
AI-Fusul al-Muhimma Uk 257


807620
captcha