Akihutubia waumini katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran Ayatullah Ahmad Jannati khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria kongamano la kimataifa la kupambana na ugaidi lililofanyika hivi karibuni mjini Tehran na kusema kuwa: “Kongamano hilo liliweka wazi mambo katika uga wa kupambana na ugaidi. Marekani na Utawala wa Kizayuni ni waungaji mkono ugaidi na walezi wa ugaidi”.
Ayatullah Jannati amekosoa kuendelea kuwepo vikosi vamizi vya Marekani katika baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati hasa Iraq na Afghanistan. Amesema vikosi hivyo vya Mareakni vimesababisha kuuawa idadi kubwa ya watu wasio na hatia.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran ameashiria hukumu iliyotolewa na mahakama ya kimataifa inayochunguza kifo cha waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri. Amesema hukumu ya mahakama hiyo imetumiwa na Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel kulipiza kisasi kushindwa kwao mbele ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika vitu vya siku 33. Amesema pamoja na njama hizo, Hizbullah imeibuka ikiwa na nguvu zaidi.
Ayatullah Jannati amesema hukumu ya mahakama ya Hariri imethibitisha kuwa mahakama hii ni kibaraka wa Marekani na Israel. Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran vilevile ameashiria matukio ya Bahrain na kukosoa kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu jinai zinazotekelezwa na utawala wa Aal Khalifa nchini humo. Amesema kosa la watu wa Bahrain ni kuwa wanataka kujiamulia mustakabali wao.
Ayatullah Jannati amesema kuwa mazungumzo kwa ajili ya maelewano ya kitaifa Bahrain ni njama ya utawala wa Aal Khalifa ya kupotosha mwamko na matakwa halisi ya wananchi. Ayatullah Jannati amesema vikosi vamizi vya Saudia lazima viondoke Bahrain mara moja.
821907