Sheikh Ahmad al Tayyib ameyasema hayo katika mazungumzo yake na ujumbe wa Wasoshalisti katika Bunge la Ulaya na akaongeza kuwa kwa kuzingatia haki zilizoghusubiwa za Wapalestina kuna haja ya jamii ya kimataifa kutazama upya misimamo yake kuhusu Israel.
Ahmad al Tayyib amesema jamii za Magharibi zinahitajia hikima na busara ya Mashariki kwa ajili ya kutatua matatizo yao. Amesisitiza kuwa nchi za Magharibi zimekuwa na siasa za kindumakuwili katika masuala yanayohusiana na Israel na ulimwengu wa Kiislamu, suala ambalo limeacha taathira mbaya katika fikra za Waarabu.
Amesema kuwa milango ya Kituo cha Kiislamu cha al Azhar iko wazi kwa ajili ya mazungumzo na makundi yote kwa sharti la kuwepo usawa na kutupiliwa mbali siasa na sera za kiimla.
Wanachama wa kundi la Wasoshalisti katika Bunge la Ulaya wamesisitiza katika mkutano huo juu ya kudumishwa uhusiano na Kituo cha Kiislamu cha al Azhar kwa ajili ya kuelewa dini ya Kiislamu. Wamesisitiza pia juu ya kufanyika mazungumzo kati ya pande hizo mbili katika siku za usoni na kupambana na hujuma inayofanywa dhidi ya Uislamu barani Ulaya. 823801