Sheikh wa al Azhar Ahmad al Tayyib amesema kuwa dikteta aliyeondolewa madarakani nchini Misri Hosni Mubarak alikuwa akiwalazimisha maulamaa wa Misri kutoa fatuwa za kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa shabaha ya kuzusha hitilafu na ogomvi kati ya Shia na Suni na kuuridhisha utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sheikh wa al Azhar amefichua baadhi ya jinai hizo za Rais wa zamani wa Misri katika kikao chake na wanaharakati wa chama al Nasiri mjini Cairo. Amesema Hosni Mubarak alikuwa akiwahamasisha maulamaa wa Kiislamu kutoa fatuwa zinazowataja Waislamu wa madhehebu ya Shia kuwa ni makafiri kwa shabaha ya kuiridhisha Israel na kuzusha mapigano kati ya mataifa ya Kiislamu.
Sheikh Ahmad al Tayyib amesema: "Hosni Mubarak alinitaka mara kadhaa nitoe fatuwa kali dhidi ya Mashia na Hizbullah ya Lebanon lakini nilikataa kufanya hivyo licha ya mashinikizo makali."
Sheikh wa al Azhar amesema ulimwengu wa Kiislamu unajifaharisha kwa kuwa na mwanajihadi mkubwa kama Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Hizbullah ambaye amesema, ameupa utawala haramu wa Israel somo kubwa ambalo kamwe hautalisahau.
Ameashiria mashinikizo makali yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wa serikali ya Mubarak ya kumlazimisha awakufurishe Waislamu wa madhehebu ya Shia na akasisitiza kuwa mashinikizo hayo yalitolewa wakati alipokuwa Mifti wa Misri na kwamba yalipungua alipokuwa Sheikh wa al Azhar ambako kulifuatana na mapinduzi ya wananchi yaliyomuondoa madarakani Hosni Mubaraka na utawala wake. 824631