Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa wapiganaji wa Hizbullah walisimama kidete kwenye maeneo yote ya kusini mwa Lebanon hata katika vijiji na kuendesha mapambano mbele ya vifaru vya jeshi la utawala wa Kizayuni, katika vita vya siku 33 vilivyoanzishwa na utawala huo dhidi ya Lebanon.
Katibu Mkuu wa Hizbullah aliyasema hayo jana kwa mnasaba wa kumbukumbu za mwaka wa tano wa ushindi wa wapiganaji wa Hizbullah katika vita vya siku 33 vilivyoanzishwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Lebanon. Sayyid Nasrullah ameashiria pia kushindwa jeshi la utawala wa Kizayuni baada ya vita vya siku 33 na kusisitiza kuwa wakuu wa usalama na kijeshi wa Israel wameitahadharisha serikali ya utawala huo kuhusu uvamizi wowote mpya dhidi ya Lebanon.
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilipata kipigo kikali katika vita lilivyoanzisha dhidi ya Lebanon mwaka 2006 na kudumu kwa siku 33 na kupelekea viongozi wa ngazi ya juu wa jeshi la Israel kujiuzulu.