Mkurugenzi wa Darul Qur'ani al Kariim katika mji wa Nasiriyya makao makuu ya mkoa wa Dhiqar huko kusini mwa Iraq, Raad Adnad al Nasiri amesema kuwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kote duniani hususan wakazi wa mji mtakatifu wa Najaf daima wanawaona Ahlusunna kuwa ni ndugu zao na kwamba kwa sasa mbali na Wasuni, wafuasi wa madhehebu za Druz, Wakristo Sabi na kadhalika wanaishi katika mji huo pamoja na wenzao Waislamu kwa amani, upendo na suluhu.
Ameongeza kuwa kuwepo Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf na mapenzi ya wanadamu kwa mtukufu huyo ndio sababu kuu ya moyo wa udugu, upendo, umoja na kuishi kwa amani kati ya watu wa mji huo.
Raad Adnan amesema kuwa wasimamiaji wa mpango wa Najaf, Mji Mkuu wa Kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu wanataka kuwathibitishia walimwengu kwamba Mashia katika kipindi chote cha historian na katika maeneo yote duniani wanataka amani, udugu na upendo kati ya wanadamu wote.
Akizungumzia historia ya mji wa Najaf Raad Adnan ameashiria kaburi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) lililoko katika mji huo na kusema mtukufu huyo alijipamba kwa sifa njema za kimaadili, uadilifu, kusaidia maskini na wasiojiweza, kupenda amani na kadhalika mambo ambayo wanadamu wote bila ya kujali dini na madhehebu zao wanapaswa kuyaiga na kuyafuata. 832397