Kwa mujibu wa kauli ya At-Twahir al-Hashimi, mwanaharakati wa Kishia wa Misri, Mashia wa nchi hiyo wanataka kusimamishwa mara moja uonyeshaji wa filamu hiyo kwa msingi wa fatuwa ya Jumuiya ya Utafiti wa Kiislamu ya Misri na Ayatullah Abbas Ka'bi, mwanchama wa Jumuiya ya Wahadhiri wa Chuo cha Kidini cha Qum.
Al-Hashimi amesema kuwa kama watu wanaohusika na urushaji hewani filamu hiyo hawataisimamisha wanahistoria wa Misri, waandishi, Jumuiya ya Masharifu wa Misri, makundi ya masufi na Jumuiya ya Ahlul Beit ya Misri watashirikiana katika kuchapisha na kusambaza kwenye vyombo vya habari vya umma, masuala ya kihistoria yanayohusiana na maisha ya Mtume na Watu wa Nyumba yake kwa kutegemea marejeo na vitabu vya Kisuni. Licha ya hayo wahusika watafikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Amewataka waandishi na wasomi wa Kiislamu katika nchi za Iraq, Lebanon, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na za kaskazini mwa Afrika kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya watu wanaohusika na utayarishaji pamoja na urushaji hewani wa filamu hiyo potofu iliyopewa jina la al-Hassan na al-Hussein (as).
Filamu hiyo inapotosha kabisa malengo na sera za maimamu wawili watoharifu waliotajwa kwa kujaribu kusafisha upotofu wa Muawiya bin Abi Sufian na mwanae Yazid. Filamu hiyo inadai kuwa maimamu hao hawakuwa na matatizo yoyote na uongozi wa watawala hao waovu.
Filamu hiyo pia inajaribu kumkosha Yazid kutokana na mauji na ukatili mkubwa alioufanya dhidi ya Ahlul Beit wa Mtume (saw) katika mkasa wa Karbala na badala yake kuelekeza lawama zote kwa Ibn Ziad na Ibn Saad. 838855