Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imelaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika mji mtakatifu wa Quds, kufuatia uamuzi wa utawala huo wa kujenga nyumba nyingine mpya 930 katika mji huo.
Akitoa taarifa kuhusiana na jambo hilo, Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo amesema kwamba hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na utawala wa Kizayuni kwa lengo la kuuyahudisha mji huo mtakatifu na kuzitaka taasisi zote za kimataifa kupinga hatua hiyo.
Katika sehemu nyingine ya taarifa yake, Ihsanoghu amesema kwamba hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa maazimio na sheria za kimataifa na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za dharura kwa lengo la kusimamisha mara moja ujenzi huo pamoja na ukandamaizaji wa utawala huo dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Nchi za Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Ulaya zimelaani hatua hiyo ya utawala haramu wa Israel. Serikali ya Tel Aviv imechukua hatua hiyo ili kupunguza malalamiko ya raia wa Kizayuni kuhusiana na mgogoro wa makazi na ongezeko kubwa la gharama ya maisha. 839916