Nassir Farid Wasil, Mufti wa zamani wa Misri amekanusha kutoa fatuwa ya kuonyeshwa sura za Maimamu wawili watukufu Hassan na Hussein (as) katika filamu iliyo dhidi ya Ushia ya 'Muawiyya, Hassan na Hussein', na kuongeza kuwa hahusiki kwa njia yoyote ile na utengenezaji wa filamu hiyo.
Mufti huyo ambaye sasa ni mhadhiri wa somo la fiqhi katika Chuo Kikuu cha kidini cha al-Azhar mjini Cairo, amesema kuwa hajatoa fatuwa yoyote ya kuruhusu kuonyeshwa nyuso za watukufu wawili hao kwenye filamu hiyo na kwamba hahusiki na utengenezaji wake. Ameongeza kuwa anaheshimu kikamilifu fatuwa ya Jumuiya ya Utafiti wa Kiislamu ya al-Azhar ambayo inazuia kuonyeshwa sura na nyuso za Manabii na maswahaba kwenye kazi yoyote ile ya kisanii au filamu ya televisheni na kukanusha habari zinazomhusisha na fatuwa iliyotajwa. Wasil amewataka Waislamu wote kuheshimu fatuwa ya jumuiya hiyo ya utafiti. Ofisi za mamarja' wa Kishia ikiwemo ya marehemu Muhammad Hussein Fadhlulla wa Lebanon (MA) na Halmashauri ya Wanazuoni wa Saudi Arabia zimepinga vikali madai ya watengenezaji wa filamu hiyo ya kashfa kwamba walipata fatuwa na vibali vya kutengeneza filamu hiyo kutoka kwa wanazuoni wa Kishia na Kisuni. 840992