IQNA

Kimya cha watawala wa Kiarabu kuhusu kesi ya Mubarak, alama ya kutokuwa na maana kesi hiyo

15:05 - August 15, 2011
Habari ID: 2170866
Kimya cha baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu kuhusiana na kesi inayoendeshwa dhidi ya Hosni Mubarak, dikteta aliyeng'olewa madarakani hivi karibuni nchini Misri ni dalili ya wazi inayothibitisha kuwa watawala hao wanaamini kuwa kesi hiyo ni ya kimaonyesho na mchezo wa kisiasa tu ambayo imekusudiwa kutuliza hali ya mambo nchini humo.
Bila shaka kama mahakama inayoendesha kesi hiyo ingefanya hivyo kwa misingi ya kisheria, bila shaka watawala hao wangepiga makelele na kulalamikia jambo hilo. Hayo yamesemwa na Muahammad Kadhim as-Shahabi, mwanaharakati wa masuala ya kisiasa nchini Bahrain anayeishi mjini London Uingereza. Hata hivyo amesema kuwa nafsi ya kuendeshwa kesi hiyo ya kimaonyesho ni hatua muhimu katika mkondo wa siasa za Mashariki ya Kati na kuonya kwamba watawala wote dhalimu na madikteta wanapasa kutambua kuwa siku itafika ambapo watawajibishwa na kutakiwa kujibu makosa na jinai walizotenda dhidi ya mataifa yao.
Akiashiria uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya Misri na mashinikizo ya madola hayo dhidi ya wanamapinduzi wa nchi hiyo, as-Shahabi amesema kuwa mashtaka yanayotajwa katika kesi ya Mubarak ni sehemu ndogo sana ya jinai na uhalifu alioufanya dikteta huyo dhidi ya taifa la Misri. Amewataka wananchi wa Mashariki ya Kati kutambua kwamba bado Marekani na utawala haramu wa Israel zina ushawishi mkubwa katika nchi za Kiarabu na kwamba hazitaruhusu watawala wapya katika nchi zilizoshuhudia mapinduzi ya wananchi kuongoza nchi zao kwa uhuru kamili.
Kwa kutilia maanani hali hiyo amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa wananchi, hasa nchini Misri, kudumisha harakati zao za mapinduzi dhidi ya watawala watakaonyesha udhaifu wa kisiasa mbele ya madola ya kibeberu ya Magharibi. 842361
captcha