Bi Bushra Khalil, wakili mwanamke aliyemtetea dikteta Saddam Hussein wa Iraq katika kesi ya mauaji na jinai dhidi ya taifa la Iraq, sasa ametangaza kuwa yuko tayari kumtetea dikteta mwingine Muammar Gaddafi wa Libya.
Amesema amechukua uamuzi wa kumtetea Gaddafi kwa sababu mashataka ambayo huenda akashtakiwa kuhusiana na nayo yanafanana sana na yale yaliyomkabili Saddam Hussein. Amesema licha ya kuwa wananchi wa Libya wanataka kumwondoa madarakani Muammar Gaddafi lakini atasimama kumtetea dikteta huyo kwa hoja kwamba wananchi hao wanaungwa mkono na jeshi la kigeni la Nato ambalo linafuatilia malengo maalumu nchini Libya.
Bi Bushra Khalil amesema baada ya kumalizika kesi ya Saddam Hussein, Gaddafi alimpongeza kutokana na ushujaa alioonyesha kwenye kasi hiyo.
Wakili huyo raia wa Lebanon amedai kwamba uadilifu haukufanyika katika kesi ya Saddam Hussein na kwamba dikteta huyo alinyongwa kutokana na mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Paul Bremer mtawala wa Marekani nchini Iraq baada ya kuangushwa utawala wa Saddam Hussein. Ameendelea kusema kuwa kwa kuzingatia hali iliyotawala nchini Iraq katika kipindi hicho hali hiyo pia itajikariri nchini Libya dhidi ya Mummar Gaddafi.
Bi Bushra Khalil amesema Marekani na washirika wake wanafuatilia mafuta na vyanzo vya uchumi nchini Libya ili kuweza kukabiliana na ushawishi unaokua kwa kasi wa China duniani. Ameongeza kuwa mafuta ya Iraq baada ya kuanguka Saddam na ya Libya baada ya kung'olewa madarakani Gaddafi yanaweza kuinusuru Marekani kutodhoofika zaidi na hatimaye kutoweka kabisa kiuchumi na kiuwezo katika uwanja wa kimataifa. 851236