IQNA

Ayatullah Isa Qassim akosoa msimamo wa kindumakuwili wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

15:54 - September 17, 2011
Habari ID: 2188422
Ayatullah Sheikh Isa Qassim, Kiongozi wa Mashia wa Bahrain amekosoa vikali msimamo wa kindumakuwili wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na mapinduzi ya wananchi yanayoendelea katika baadhi ya nchi za Kiarabu katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Akizungumza jana katika hotuba za Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Swadiq (as) huko katika mji wa Diraz nchini Bahrain, Sheikh Qassim ameikosoa vikali jumuiya hiyo kutokana na misimamo yake ya upendeleo na ubaguzi dhidi ya mapinduzi na mwamko wa Kiislamu wa wananchi katika baadhi ya nchi za Kiarabu na kuwataka wanachama wa jumuiya hiyo kuchukua msimamo thabiti na imara katika kukabiliana na jinai na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Bahrain dhidi ya wananchi wasio na hatia wa nchi hiyo kwa ushirikiano wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia.
Wakati huohuo ameutaka utawala wa Bahrain kuheshimu haki za kimsingi za Wabahrain na kutowabagua kwa misingi ya kimadhehebu na kisiasa.
Sheikh Qassim amesisitia juu ya kuheshimiwa haki na matakwa ya Mashia wa Bahrain ambao ndio wanaounda sehemu kubwa ya raia wa nchi hiyo. 861980
captcha