Hii leo Wamagharibi ambao wamekuwa wakiwadhalilisha Waislamu na kudai kwamba hawafahamu chochocte kuhusiana na suala la demokrasia wamelazimika kubadili mtazamo huo baada ya kushuhudia wimbi kubwa la mwamko wa Kiislamu katika nchi zilizotajwa, mwamko ambao umetimia kupitia mapinduzi ya wananchi wanaopigania haki zao za kimsingi kutoka kwa watawala madhalimu wanaoungwa mkono na madola ya kibeberu ya Magharibi.
Hayo yamesemwa na Hujjatul Islam wal Muslimeen, Mahdi Mudarrisi, Mkurugenzi wa Idhaa ya Ahlul Beit (as) inayorusha hewani matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza kutokea mjini London. Ameyasema hayo alipokuwa akihutubia hapo jana Jumatatu kikao cha tano cha Baraza Kuu la Muungano wa Idhaa na Televisheni za Kiislamu unaoendelea mjini Tehran Iran. Amesema wimbi hilo la mwamko wa Kiislamu ambalo limeshamiri dunia nzima, limefikia kiwango cha utendaji na kwamba hivi sasa mataifa yanataka kueneza haki na kuvunja batili. Sayyid Mahdi Mudarrisi amesema kuwa jukumu zito la Manabii wa Mwenyezi Mungu lilikuwa ni kuwaamsha waliolala na kwamba Bibi Fatuma (as) binti wa Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) pia alikuwa akiwatahadharisha mara kwa mara Waislamu dhidi ya kulala.
Ameashiria harakati za mapinduzi zinazofanywa na wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala dhalimu wa ukoo wa Aal Khalifa wa nchi hiyo na kusema kuwa harakati hizo zimeingia katika hatua mpya ambapo wanawake wanaonekana wakiwa katika mstari wa mbele wa harakati hizo za amani lakini utawala wa Manama umekuwa ukikabiliana nao kwa njia ya kinyama kabisa kwa kuwakandamiza na kuwatendea jinai ambazo zilikuwa hazijawahi kuonekana katika nchi za Kiarabu katika siku za hivi karibuni. 867913