Akizungumza katika kikao hicho hapo jana alasiri, Rais Ahmadinejad ameashiria umuhimu wa vyombo vya habari katika kufikisha ujumbe wa uadilifu na usawa kwa walimwengu na kuongeza kuwa mwanadamu ana umuhimu mkubwa kwa sababu ulimwengu mzima umeumbwa kwa ajili yake yeye. Kwa msingi huo amesisitiza kwamba mtazamo wa vyombo vya habari vya Kiislamu unapaswa kurekebishwa kwa ajili ya kuishughulikia jamii nzima ya mwanadamu ili kuboresha maisha yake ya humu duniani na ya huko Akhera. Amesema mtazamo wa vyombo hivyo vya habari unapasa kuwa wa kimataifa na sio wa kieneo tu.
Rais Ahmadinejad amesema ushindi wa mwisho katika uwanja wa upashaji habari utakuwa wa chombo cha habari ambacho kitafanikiwa kuvutia fikra za waliowengi kimataifa na sio kieneo tu. Amesema, Waislamu wana lengo la kueneza mwamko wa Kiislamu duniani kote ili mataifa yanayodhulumiwa na madola makubwa ya kibeberu na ya kikoloni yaweze kuamka na kupigania haki zao za kimsingi. Rais Ahmadinejad amesema, ulimwengu unapasa kutawaliwa na fikra ya Tauhidi uchaji-Mungu pamoja na uadilifu na sio dhulma na jinai zinazotekelezwa dhidi ya mwanadamu na madola ya kibeberu ya nchi za Magharibi. Ameendelea kusema kuwa nchi za kibeberu za Magharibi zimefikia mwisho wao kutokana na sera zao batili za umaada na ubepari na kwamba hii leo ulimwengu unasubiri kunufaika na ujumbe mpya unaomletea mwandamu saada na ukamilifu, ujumbe ambao si mwingine bali uliosimama juu ya msingi wa uadilifu na usawa.
Vilevile amesisitiza kwamba hakuna ujumbe mwingine wowote ulio juu ya huo kwa thamani, ukamilifu na ubora.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaka Muungano wa Idhaa na Televisheni za Kiislamu kupanga mipango madhubuti ya kuuwezesha kuwa na nafasi muhimu katika ufikishaji ujumbe huo kwa jamii ya mwanadamu duniani. 869553