Msikiti mtukufu wa al-Aqsa, ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu, unakabiliwa na jinai kubwa zaidi ya Wazayuni katika historia yake.
Wazayuni wangali wanaendelea kuchimba mashimo na njia za chini kwa chini katika msikiti huo jambo linalohatarisha uimara wake.
Hayo yalisemwa jana alasiri na Ahmad Bahar, Naibu Spika wa Bunge la Palestina anayeshiriki katika kikao cha tano cha mkutano wa kimataifa wa uungaji mkono kwa taifa la Palestina unaofanyika mjini Tehran. Amesema katika kipindi chote cha Intifadha ya Palestina majeruhi na mashahidi wa Kipalestina wametoa damu ambayo imedhamini usalama wa Quds Tukufu na Palestina nzima kwa ujumla. Amesema Intifadha hiyo bado inaendelea na kwamba Wapalestina hawatapumzika hadi pale watakaporejesha ardhi zao zote kutoka kwenye makucha ya walowezi wa Kizayuni.
Ahmad Bahar amesema kwamba Msikiti wa al-Aqsa unakabiliwa na hali mbaya zaidi katika historia yake kutokana na vitendo vya kibaguzi vinavyotekelezwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina. Ameongeza kuwa hii leo msikiti huo mtukufu unakabiliwa na hatari ya kuporomoka kabisa kutokana na uchimbaji haramu unaofanywa na Wazayuni chini ya msikiti huo kwa madai ya kujenga hapo hekalu lao.
Naibu Spika wa Bunge la Palestina amesema Mayahudi wamekuwa wakifanya sherehe potofu katika msikiti huo ili kufuta utukufu wake wa Kiislamu. 871180