Akizungumza hapo jana Jumaosi kupitia televisheni ya Misri, Clinton amedai kwamba serikali ya Washington iko tayari kushirikiana na serikali yoyote ile itakayobuniwa Misri hata kama itakuwa ya Kiislamu lakini kwa sharti kwamba iheshimu kile alichokitaja kuwa uhuru na sheria na kupinga vitendo vya mabavu.
Clinton amedai kwamba tokea mwanzoni mwa mapinduzi hayo serikali ya Marekani iliwasiliana na watawala wapya wa kijeshi wa Misri na kuwataka wajiepushe kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Amesema anaunga mkono kudumishwa kwa misaada ya kijeshi na isiyo ya kijeshi ya Marekani nchini Misri na kuyasihi mashirika binafsi ya Marekani yanayoendesha shughuli za kiraia nchini humo yaendelee na shughuli hizo bila kuhofu lolote.
Amesema Wamarekani wanashangazwa na mambo yanayoendelea Misri lakini akaongeza kuwa watawala wa nchi hiyo wanafahamu hali ngumu inayoikumba nchi hiyo kwa sasa.
Matamshi hayo ya Clinton yanapingana wazi wazi na matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa katika siku za hivi karibuni na viongozi pamoja na maafisa wengine wa Marekani, ambapo wamesikika wakisema kwamba Marekani haikupendelea kuona mapinduzi hayo ya wananchi yakitokea Misri, na ndio maana wakachukua muda mrefu kabla ya kukiri kwamba dikteta Hosni Mubarak, muitifaki mkubwa wa Marekani, alikuwa amepoteza udhibiti wa nchi hiyo ya Kiarabu. 871515