Bitawi amesema kitendo hicho ni jinai inayotekelezwa kwa misingi ya kibaguzi na kwamba ni aina ya ugaidi dhidi ya Wapalestina.
Bitawi ambaye pia ni mbunge katika bunge la Palestina amesema kwamba kitendo hicho ni kuendelezwa jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya misikiti, makaburi na maeneo ya ibada ya Wapalestina. Amesema jinai hiyo inakiuka sheria za kimataifa na dini zote ambazo zinasisitiza udharura wa kuheshimiwa maeneo ya ibada na matukufu ya dini zote za mbinguni.
Bitawi amewataka Wapalestina wote kusimama imara dhidi ya jinai hizo za Wazayuni na kufanya kila wawezalo kwa ajili ya kutetea matukufu yao ya kidini.
Askari wa utawala ghasibu wa Israel walibomoa Msikiti wa Yazra jana alfajiri kwa kisingizio kuwa umejengwa karibu na eneo moja la kijeshi ambapo ujenzi haupasi kufanyika.
Hii ni katika hali ambayo vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi vinazidi kujengwa katika eneo hilo bila kukabiliwa na tatizo lolote.
Utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha kampeni maalumu ya kuharibu misikiti ya Wapalestina katika eneo hilo ili kuliunganisha na ardhi nyinginezo za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu. 878301